Monday, May 6, 2019

TUCHANGAMKIE FURSA YA VIFUNGASHIO - MGALU

WANANCHI katika vijiji vinavyounda halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wametakiwa kuchangamkia fursa ya kufungiwa kwa mifuko ya plastiki, kwa kutengeneza vikapu vya asili, vitakavyochukua nafasi ya mifuko ya plastik.


Kufungiwa kwa mifuko hiyo kunakoelezwa ni hatua ya kupambana na uchafuzi wa mazingira, kunatokana na mifuko hiyo kutooza haraka iwapo ardhini, licha ya kuwa msaada kwa wananchi katika kubebea vitu mbalimbali.


Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa viti maalum, mkoa wa Pwani, Subira Mgalu, alipozungumza na wajasiriamali katika vijiji vilivyopo Kata za Talawanda na Kiwangwa, ambao wamekopeshwa fedha za asilimia zilizotolewa na halmashauri ya Chalinze, wilayani hapa.


Alisema kwamba serikali iliyopo madarakani kupitia wizara husika ya mazingira, imefanya utafiti wa kina hivyo kubaini uwepo wa uchafuzi wa mazingira, na kufika hatua ya kufungia mifuko hiyo, inayolenga kupambana na hali hiyo.


"Tuchangamkie fursa ya kutengeneza vikapu vyetu vya asili, ukiangalia kwa haraka unaweza kusema kufungiwa kwa mifuko kutatuathiri katika uchukuzi, hii imeturejeshea fursa ya kibiashara ya kutengeneza vikapu, ambavyo wazee wetu walikuwa wanavitengeneza," alisema Mgalu.


"Miyaa, ukindu na rangi vyote tunavyo, kilichobaki sasa ni kuitumia fursa hii kutengeneza vikapu kwa wingi, kisha tuvipeleke katika maeneo mbalimbali ninaimani kubwa kwamba hatua hii imeleta neema kwetu," alisema.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze Said Zikatimu alisema kwamba, wanaendelea na ukopeshaji wa vikundi vya ujasiriamali, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali kuvikopesha vikundi mikopo isiyokuwa na riba.


"Katika halmashauri yetu fedha sio tatizo, tunazo za kutosha, tunachokiomba kutoka kwenu ni kuanziasha vikundi, kuvisajili kisha kuwasilisha kwenye ofisi ya Maendeleo ya Jamii ili muweze kunufaika na mikopo hiyo isiyo na riba," alisema Zikatimu.

No comments:

Post a Comment