Tuesday, May 28, 2019

WASICHANA WAJENGEWA UWEZO NA ROOM TO READ.

 Meneja wa Mradi wa elimu kwa msichana chini ya Taasisi ya Room to read, Zamaradi Saidi, akizungumza na wasichana, wanafunzi wa shule ya Sekondari Chalinze.
 
Meneja wa Mradi wa elimu kwa msichana chini ya Taasisi ya Room to read, Zamaradi Saidi, alipokuwa akizungmza na mwandishi wa BAGAMOYO KWANZA BLOG.
...................................... 

Taasisi ya Room to read Tanzania imeandaa semina kwa wasichana wanaosoma shule za sekondari Mkoani Pwani ili kuwajengea uweza wa maarifa ya vitu vya kufanya baada ya kumaliza masomo.


Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa kufungua semina hiyo, Meneja wa Mradi wa elimu kwa msichana chini ya Taasisi ya Room to read, Zamaradi Saidi, amesema wamekuwa wakiandaa semina kama hizo za ujasiriamali kwa wasichana ili watakapomaliza masomo yao waweze kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira.


Alisema jamii imejenga mazoea ya kusubiri kazi za kuajiriwa hali inayopelekea hata kijana aliyemaliza elimu ya chuo kikuu anashindwa kuendesha maisha yake mpaka apate kazi ya kuajiriwa.


Alifafanua kuwa, kufuatia dhana hiyo iliyojengeka katika jamii, Taasisi ya Room to read imekuja na mpango wa elimu kwa msichana ambao ndani yake wasichana wanafundishwa mbinu za kujiajiri.


Alisema kuwa, Room to read imekuwa ikitafuta walimu wa aina mbalimbali wa ujasiriamali ili wasichana hao pamoja na elimu ya sekondari wanayopata wawe na elimu ya ziada ya kujiajiri pindi wanaposhindwa kuendelea na masomo au kukosa kazi za kuajiriwa.


Aidha, aliongeza kuwa, elimu wanayopata wasichana hao tayari watakuwa na uhuru wa kuchagua aina tatu za mfumo wa maisha ili kuendesha familia zao.


Alizitaja aina hizo tatu za mfumo wa maisha kuwa ni kujiajiri, kuajiriwa na kujiajiri pamoja na kuajiriwa, ambapo uhuru huo wa kuchagua haupatikani ispokuwa kwa mtu ambae tayari amejitosheleza katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu ya darasani na ujasiriamli.


Alifafanua kuwa, Mradi wa elimu kwa msichana ambao ndani yake kuna elimu ya fedha na ujasiriamali, umelenga kumfanya msichana atambue kuwa, anaweza kujiajiri, kuajiriwa au vyote kwa pamoja.


Aliendelea kusema kuwa, miongoni mwa elimu wanazopata wasichana hao kupitia wawezeshaji wa semina hizo ni pamoja na nidhani ya matumizi inayokwenda sambamba na uadilifu katika matumizi.


Alisema mtu yeyote ili aweze kufanikiwa kuanzisha au kuendeleza mtaji ni lazima awe na uadilifu katika matumizi ya fedha na sio kutumia bila ya mpangilio.


katika semina hiyo iliyofanyika shule za skeondari Matimbwa na Chalinze wawezeshaji wa aina mbalimbali wamealikwa kwaajili ya kufikisha masomo ya ujasiriamali sambamba na uwekaji akiba kwaajili ya kuanzisha na kuendeleza mitaji.


Wawezeshaji kutoka Benki ya NMB wameweza kutoa somo la umuhimu wa kuweka akiba kwaajili ya kutimiza malengo mbalimbali ya kujiendeleza.


Waliwaeleza wasichana hao kuwa, ili kuweza kufanikiwa katika malengo mbalimbali lazima kuwa na nidhamu ya fedha ambapo unapaswa kujua mapato, matumizi, faida na hasara.


Kwa upande wao wasichana waliopata elimu hiyo kutoka shule ya Sekondari Chalinze na Matimbwa wilayani Bagamoyo, walisema wamefaidika sana na elimu hiyo ambayo imewatoa gizani.


Walisema kwa sasa wanajua kuanzisha biashara, kutafuta masoko na namna gani kuandaa bidhaa ili mteja iweze kumvutia.


Mradi wa elimu kwa msichana chini ya Room to read Tanzania umejikita katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuwasaidia wasichana wanaotoka kwenye mazingira magumu msaada wa vifaa vya shule, kuwapa stadi za maisha wasichana wote, kuwapa ushauri wa jumla kuhusu maisha yao ya shule na baada ya shule.


Hata hivyo elimu hiyo inaendelea pia kwenye jamii ambapo Room to read hufanya semina na wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ili kuwaeleza umuhimu wa kumsaidia msichana kuweza kumaliza elimu yake ya sekondari na kupata stadi muhimu ambazo zitamsadia kufanya maamuzi sahihi za maisha yake.

 Muwezeshaji, Richard kutoka NMB akisisitiza  jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa kuweka akiba.
 
Muwezeshaji, Rashid Shomvi, kutoka NMB akiwasilisha mada kuhusu nidhamu ya matumizi ya fedha, semina hiyo iliandaliwa na Room to read na kufanyika Shule ya Sekondari Chalinze.

 
Wasichana, wanafunzi wa shule ya Sekondari Chalinze, wakinyoosha mikono kama ishara ya kuelewa somo lililofundishwa na muwezeshaji.

No comments:

Post a Comment