Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ya
Bagamoyo, Zainabu Kawawa ametoa rai kwa Wananchi wa Bagamoyo, hususani
Wazee, kujiunga na mfuko wa Afya ya jamii (CHF) iliyoboreshwa, ili iwasaidie
kumudu huduma za matibabu pale wanapozihitaji.
Kawaw, ameyasema hayo, hivi karibuni alipokuwa katika hafla maalum ya uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho vya matibabu bure kwa wazee 2000 wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
“Wazee wangu mliofika hapa leo na Wananchi wote wa Bagamoyo, ni vema wote tukumbuke kwamba maradhi huwa hayabishi hodi, na huja bila taarifa, litakuwa jambo la kheri yatakapotufikia tuwe tumejipanga vizuri kwa kuhakikisha kila mmoja wetu amejiunga na mfuko wa Afya ya jamii kupitia mpango wa CHF iliyoboreshwa ambapo itakugharimu kiasi cha Shilingi 30,000/= tu, Mwaka mzima" Alisema.
"Kadi hii ya CHF iliyoboreshwa itakuwezesha kupata huduma bora za afya bure wewe
na wategemezi wako 6, katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya, Zahanati,
Hospitali ya Wilaya na Hospitali kuu ya Mkoa” Aliongeza Kawawa.
Nae mratibu wa dawati la Wazee, kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Rajabu Mturuya katika taarifa yake aliyosoma mbele ya mgeni rasmi amesema, katika kipindi cha Januari – Machi 2019 Idara ya Afya kupitia Kitengo cha Ustawi wa Jamii iliwapiga picha Wazee 2000 katika kata za Dunda, Magomeni, Nianjema, Kisutu, Kiromo, Zinga, Makurunge, Yombo na Fukayosi.
Aliongeza kuwa, katika
kipindi cha Oktoba – Desemba 2018 kata za Kerege na Mapinga jumla ya Wazee
waliopigwa picha ni 349 ikiwa ni hatua ya kwanza ya kuandaa vitambulisho vya
matibabu ya wazee.
Alisema hadi kufikia sasa Halmashauri ya Wilaya kupitia Idara ya Afya, imetoa jumla ya vitambulisho 750 kwa Wazee ambavyo wameanza kuvitumia kwa ajili ya kupata matibabu katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya ndani ya Wilaya, hadi kufikia mwezi Juni 2019 Halmashauri inatarajia kutoa vitambulisho 2,000 kwa Wazee wote waliopigwa picha.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainab Kawawa amezindua bodi mpya ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambayo imeanza kazi tangu tarehe 13.03.2019 na inatarajiwa kutekeleza majukumu yake kwa muda wa miaka mitatu hadi tar. 13.03.2022.
Mkuu huyo wa wilaya ameitaka bodi hiyo mpya kuhakikisha inasimamia vyema uboreshaji wa
utoaji wa huduma za Afya, ili Wananchi wanufaike na uboreshaji wa utoaji wa
huduma za Afya uliofanywa na Uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, Chini ya
Mhe. Rais, Dkt. John Joseph Magufuli, iliyoleta mapinduzi makubwa katika sekta ya
Afya kwa kujenga vituo vipya vya Afya, Hospitali za Wilaya na utoaji wa dawa na
vifaa tiba katika Halmashauri zote Nchini.
“Nendeni mkasimamie utoaji wa huduma bora za Afya, Hakikisheni Wazee na Wananchi wote kwa ujumla, wakifika katika vituo vya kutolea huduma wanapokelewa vizuri, hawasumbuliwi na wanapatiwa huduma stahiki kwani Sekta ya Afya ni Sekta yenye changamoto nyingi sana katika masuala ya utoaji huduma na muwe na ushirikiano ili sote kwa pamoja tuhakikishe huduma a Afya kwa Wananchi wa Bagamoyo zinaboreka.
Bodi mpya ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo inaundwa na wajumbe 6 ambapo inaongozwa na Mwenyekiti Bi. Roswita F. Kasikila ambaye amemuahidi Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo na Wananchi wote wa Bagamoyo kuwa itafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, kanuni na miongozo iliyopo, kusimamia na kuhakikisha huduma za Afya ndani ya Halmashauri zinatolewa kwa ufanisi na weledi.
“Tutasimamia uanzishwaji wa dirisha la kuhudumia Wazee, tutashirikiana na Mkurugenzi, kupitia uongozi wa Idara ya Afya kuhakikisha kila kituo cha kutolea huduma za Afya kinaanzisha dawati la kuhudumia Wazee, ili Wazee wasiendelee kupata usumbufu wanaoupata sasa wanapofika katika Vituo vya Afya kupata huduma” Alisema Bi. Roswita Kasikila.
Bodi ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ina wajibu wa Kuhakikisha jamii inapata huduma bora za Afya inazozimudu, na zinazoimarisha Afya zao, kujadili na kurekebisha mipango ya Afya na bajeti kisha kuwasilisha kwa Halmashauri kwa ajili ya kuidhinishwa, kupokea, kuchambua na kuidhinisha taarifa za utekelezaji kutoka kwa Timu za uendeshaji wa Huduma za Afya Halmashauri, kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato na kukusanya rasilimali za kutosha kuendesha huduma za Afya za Halmasahuri na kusaidia timu za uendeshaji wa huduma za Afya.
No comments:
Post a Comment