Saturday, May 11, 2019

KATIBU WA CCM ATOA TAMKO RUFIJI.

Na Shushu Joel, Ikwiriri.


KATIBU wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Omary Mtuwa ametoa onyo kali viongozi na wanachama wa chama hicho wenye tabia ya kujifanya CCM mchana na huku usiku ni wapinzani.


Akitoa onyo hilo Mtuwa alisema kuwa kuna taarifa kuwa baadhi ya viongozi na wanachama CCM wamekuwa na tabia za kukisaliti chama kwa kuwafanyia wapinzani kampeni kipindi cha usiku na kuwapatia taarifa juu ya kile kinachopangwa kwenye vikao vya CCM kuhusu mwelekeo wa ushindi.


Onyo hilo  amelitoa jana wakati wa mkutano na viongozi wote wa kata, matawi na mashina uliokuwa na lengo la kupeana mikakati ya ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu nchi nzima.


"Sasa nawatahadharisha mapema kuwa mtu yeyote yule tutakaye mbaini na tabia hiyo cha moto lazima akione juu yake na lazima ajutie jambo hilo"Alisema.


Aliongeza kuwa Rufiji ilikuwa ngome ya Cuf lakini tangu kuanza kwake kazi wamekuwa na kazi ya kupokea wanachama wa upinzani toka maeneo mbalimbali ya wilaya.


Aidha amewataka viongozi hao kuhamasisha wanachama kulipia ada zao ili utambulisho wao uendelee kuwepo ndani ya chama hicho.


Pia katibu huyo amewataka wana CCM wa Rufiji kutembea kifua mbele kutokana na jinsi hali ya machafuko ilivyokuwa kipindi cha nyuma lakini Mwenyekiti wa CCM Taifa Comred Dkt John Pombe Magufuli amelimaliza na sasa kila jambo ni shwali katika wilaya yetu.


Aliongeza kuwa kutokana na jinsi gani Mwenyekiti wetu wa taifa alivyojitolea kulimaliza jambo hilo sie kama wanarufiji tunampatia Zawadi ya ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa asilimia 95 kama pongezi kwetu juu ya jambo alilotufanyia.


Kwa upande wake katibu mwenezi wa kata ya mgomba Fatma Mohamed amempongeza katibu huyo kwa kuwakutanisha viongozi na baadhi ya wanachama kwa lengo la kujadili mustakabali wa chama Chao na hasa wale wenye tabia ya kuwa wasaliti wa chama hicho.


Aidha amewataka viongozi wenzake kutembea kifua mbele kwani ni makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya tano hivyo ushindi ni lazima upatikanaji kwa kishindo.


Naye Mbunge wa jimbo hilo Mohamed Mchengelwa amewapongeza viongozi hao kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo na hii ni ishara kubwa hakuna kizingiti cha aina yeyote ile katika uchaguzi wa serikali za Mitaa.


Pia amewataka viongozi hao wa ccm kuyasemea yale yote yanayofanywa na Rais Magufuli katika jimbo hilo kwani ni mengi sana.


Aidha amewahakiishia wananchi kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli ipo makini katika kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanafanyika kwa haraka ili wananchi waweze kunufaika na miradi yao.

No comments:

Post a Comment