Sunday, May 5, 2019

JUMAA AISHUKURU TAMISEMI, AISHAURI.

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, (kulia) akiwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Butamo Ndalahwa, wakikagua majengo hayo, Picha na Omary Mngindo.
...................................... 

Na Omary Mngindo, Mlandizi 


MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, ameishukuru Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa fedha kiasi cha sh. Bil. 1.5 zinazojenga hospitali ya wilaya. 


Jumaa ametoa shukrani hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea ujenzi wa hospitali hiyo, inayojengwa katika Kitongoji cha Disunyala, Kata ya Kilangalanga, akiambatana na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Butamo Ndalahwa ambapo amejionea maendeleo mazuri ya ujenzi huo. 


Aidha Jumaa ameishauri Wizara hiyo kwamba inapozipatia fedha halmashauri, basi iziache zijipangie wenyewe namna watavyojenga majengo, kulingana na eneo walilonalo, ikiwa wataweza kujenga ghorofa au majengo yatakayoendana na ardhi ya sehemu husika. 


"Mfano wa ushauri wangu nautolea hapa, hili eneo ni kubwa lakini kutokana na kujengwa majengo mbalimbali, hapa katikati imeachwa sehemu ambayo kimsingi haina faida, kwani haiwezi kutumika kwa ujenzi wowote, tungeachiwa tungejenga ghorofa ardhi kubwa ingebaki," alisema Jumaa. 


Aidha mbunge huyo ameridhishwa na kasi ya ujenzi, japokuwa kunajitokeza changamoto za hapa na pale, zinazochangia kusuasua kwa ujenzi huo unaoelekea ukingoni, huku akiwataka wanaosimamia kazi hiyo kuendelea na kazi ili ikamilike kwa wakati muafaka.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Butamo Ndalahwa aliwambia waandishi wa habari kwamba, wameitumia siku ya upandaji miti, ambapo katika eneo hilo amepanda miti 1,200 lengo ni kuweka mipaka ya eneo lenya eka 42. 


Akizungumzia ujenzi huo, Ndalahwa alisema kuwa baada ya serikali kuwapatia kiasi cha sh. Bil. 1.5 za ujenzi wa majengo matano ya awali, tayari wameshapaua maabara, chumba cha mionzi wakati duka la dawa wanasubiri vifaa maalumu vinavyotunzia ubaridi. 


"Majengo ya Utawala, wagonjwa wa nje, kufulia na wodi kwa ajili ya wazazi hayo tunataraji kuyapauwa wiki ijayo, juu ya changamoto za upatikanaji wa vifaa, tumeshaifanyiakazi kwa kuvileta eneo la tukio wiki moja kabla ya kuhitajika," alisema Ndalahwa. 


Mkurugenzi huyo alimalizia kwa kusemaa kwamba, kazi hiyo ya upauaji inataraji kumalizika kwa wakati ambapo mwezi huu wa tano itakuwa imekamilika, huku akiwashukuru mafundi na wasimamizi wa kazi hiyo kwa juhudi zao.
 
 MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, akitumia futi kamba kupima urefu wa ukuta wa moja ya majengo ya Hospitali ya wilaya ya Kibaha wakati alipotembelea kukagua ujenzi unavyoendelea.
    
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, akipima urefu wa dari ili umbali utakaofungwa feni katika moja ya majengo ya Hospitali ya wilaya ya Kibaha wakati alipotembelea kukagua ujenzi unavyoendelea.

No comments:

Post a Comment