Saturday, May 18, 2019

ROOM TO READ YAWEZESHA WASICHANA KUJIFUNZA UJASIRIAMALI.

Afisa mradi wa elimu ya fedha chini ya mpango wa elimu kwa msichana kutoka shirika la Room to Read, Bi Rehema Juakali, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati walipotembelea kiwanda cha mjasiriamali mwanamke wa Bagamoyo Teddy Davis.
 
Mwenyekiti wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Bagamoyo, Teddy davis, akizungumza na waandishi wa habari kiwandani kwake Nianjema Bagamoyo alipotembelewa na wanafunzi wa shule ya sekondari Matimbwa ambao walifika hapo kujifunza ujasiriamali.
................................



Shirika lisilo la kiserikali la  Room to read nchini Tanzania limeendelea kumuwezsha msichana kielimu ambapo kupitia mradi wa elimu ya fedha, wasichana wengi wameweza kunufaika kwa kupata elimu ya utunzaji wa fedha, kukuza mitaji na hatimae kuweza kujiajiri kupitia elimu hiyo ya fedha chini ya mradi wa elimu kwa msichana.


Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Afisa mradi wa
elimu ya fedha chini ya mpango wa elimu kwa msichana kutoka shirika la Room to Read, Bi Rehema Juakali walipokuwa kwenye ziara ya kimasomo na wasichana wa shule ya Sekondari Matimbwa ambapo walitembelea kiwanda cha Mjasiriamali wa Bagamoyo Tedy Davis ili kuona namna mwanamke anavyoweza kujitegemea kwa kutumia ujasiriamali wa vitu mbalimbali.


Alisema shirika hilo limeandaa mitaala maalum ya kufundishia ujasiriamali ikiwa ni pamoja na misingi mikuu ya ujasiriamali huku wanafunzi wakipata nafasi ya kwenda kwenye ziara za kimasomo nje ya shule ili kujifunza mambo mbalimbali kwa uhalisia wake.


Juakali, alisema mradi wa elimu ya fedha ni mradi ulionzishwa rasmi mwaka 2018 kwa shule zinazofadhiliwa na shirika la Room to Read ili kuwajengea uwezo wasichana katika maswala ya kifedha na uchumi kwa ujumla.


Aliongeza kuwa, mpaka sasa shule kumi zimepata fursa ya kupata mradi huo ambazo Halmashauri ya Bagamoyo ni shule nne Chalinze shule mbili huku Kibaha kukiwa na shule nne.


Alisema shule hizo kumi ni wanufaika wakubwa wa mradi wa elimu ya fedha ambapo wanafunzi wake wameweza kuwa na mabadiliko ya kitabia na kiuchumi hasa katika kujiwekea akiba ya fedha na hatimae kuweza kujifanyia mambo mbalimbali ya maendeleo katika familia zao.


Aliendela kusema kuwa, kwa wasichana wa ngazi ya sekondari tayari wamekuwa na uwezo wa kuandaa mpango wa biashara (Business plan) na kufahamu mbinu za kukuza mitaji na kuvutia wateja katika biashara husika.


Nae Mwalimu muwakilishi wa mradi wa elimu ya fedha, Jamila Kaniki, amesema mradi huo umewasaidia wasichana kujitambua na kuwa na uwezo wa kufikiri mambo ya maendeleo.


Alisema  elimu hiyo inamfanya msichana aweze kufikia malengo yake jambo ambalo kwenye mitaala ya kawaida halipo.


Aliongeza kwa kusema kuwa, inamfanya msichana kuwa na uwezo wa kujiamini hali iliyopelekea kupungua kwa mimba za utotoni.


Mwalimu Jamila, aliongeza kwa kusema kuwa, vijana wengi baada ya kumaliza masomo na kukosa nafasi za kazi huingia mitaani na kujiunga na makundi yanayokwenda kinyume na maadili lakini kwa msichana aliyepata elimu ya fedha chini ya mpango wa elimu kwa msichana kutoka shirika la Room to Read ni rahisi kwake kujiajiri na kuendesha maisha yake.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Bagamoyo, Teddy davis ambae ndie mjasiliamali aliyetembelewa na wanafunzi hao alisema wasichana wanapaswa kuwa na ndoto ya mafanikio na kwamba haifai kukata tamaa na kujiona kama hawawezi.


Teddy ambae alishinda tunzo ya Malkia wa nguvu 2018 kutoka Bagamoyo alisema yeye alithubutu akaweza hivyo anaamini kila mwanamke anaweza kufikia malengo yake.


Alisema wasichana wanapokosa alama za kuendelea kimasomo wasikate tamaa na badala yake watumie fursa ya kujifunza ujasiriamali ili waweze kutimiza ndoto zao za maisha.


Aliongeza kuwa, kufeli masomo sio kufeli maisha, hivyo mwanafunzi anaweza kufeli masomo lakini akafaulu maisha kupitia ujasiriamali.


Teddy alisema anafikiria kuomba fursa ya kufundisha elimu ya ujasiriamali katika shule mbalimbali ili kuwajengea uwezo wasichana waweze kujiamini na kuwa na elimu ya kuendesha maisha yao mara tu wanapomaliza masomo yao.


Kwa upande wao wanafunzi wa shule ya Sekondari Matimbwa wamefurahia ziara hiyo ya kimasomo na kusema kuwa wamejifunza vitu vingi kupitia mjasiriamali Teddy.


Aidha, wakizungumzia elimu ya fedha wanayopata kupitia mpango wa elimu kwa msichana kutoka shirika la Room to Read, wanafunzi wa shule ya Sekondari Matimbwa iliyopo wilayani Bagamoyo, wamesema wamenufaika sana na kwamba nao wanaweza kuiendeleza elimu hiyo kwa jamii.
  
Mwalimu muwakilishi wa mradi wa elimu ya fedha, Jamila Kaniki akizungumza na waandishi wa habari wakati walipotembelea kiwanda cha mjasiriamali mwanamke wa Bagamoyo Teddy Davis.
 
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Matimbwa wakisikilza elimu ya ujasiriamali walipotembelea katika kiwanda cha mjasiriamali Teddy Davis mjini Bagamoyo.
    
Mkurugenzi wa kiwanda cha Smoke Hause StoreTeddy Davis Teddy Davis akitoa elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Matimbwa Bagamoyo ambao walifika kujifunza kiwandani hapo.


No comments:

Post a Comment