Monday, May 20, 2019

BIL. 29 KUMALIZA TATIZO LA MAJI CHALINZE

Na Omary Mngindo, Ubena


RAIS Dkt. John Magufuli amesikia kilio cha wananchi wa jimbo la Chalinze, wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kinachohusu tatizo la maji, ambapo ametenga kiasi cha sh. Bil. 29 kwa ajili ya mradi mpya wa maji kutoka Ruvu kwenda Chalinze.


Mradi huo unaolenga kuwasaidia wananchi hao ambao kwa miaka mingi wamekuwa katika adha hiyo, pia unatarajiwa kufika katika maeneo ya Msata, Mdaula, Msolwa, Ubena, Tukamisasa na kwenda njia ya jeshini kata ya Ubena.


Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete, alipokuwa anazungumza na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ubena, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wakiwemo Wajasiriamali wa vikundi mbalimbali na waendesha bodaboda.


Alisema kuwa alifikisha kilio hicho kwa Rais Dkt. Magufuli kuhusiana na adha hiyo, ambapo amekubali kisha kutenga kiasi hicho cha fedha zitakazokwenda kufanikisha mradi huo, utakaoambatana na kuiua Chaliwasa kisha kutengeneza Mamlaka moja pamoja na Dawasa.


"Hayo yote anayoyafanya Rais Magufuli inatokana na thamani tunayompa sisi wana-Chalinze, lakini si mimi Mbunge ninayeifanya kazi hiyo, bali na nyinyi ambao kwa umoja wetu tunafanikisha masuala mbalimbali ya kimaendeleo, pia tunajukumu la kutangaza kazi nzuri inayofanywa na Chama Cha Mapinduzi," alisema Ridhiwani.


Alisema kuwa ifike wakati vikundi vinavyopatiwa pesa vitambue kwamba, havipewi kwa sababu wamewachagua, bali serikali ya Chama Cha Mapinduzi inataka kuona mabadiliko ya maisha ya watu wake, huku akitolea mfano vikundi vya bodaboda vinaongeza mifuko yao, pia wakulima watanunua pembejeo za kisasa pamoja na mbolea.


Kuhusu changamoto ya maji inayoikabili jimbo hilo, Ridhiwani alisikitishwa kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi zinazodai kwamba, kati ya 2010 mpaka 2015 ndoa nyingi zimepata matatizo, chanzo kikubwa kikiwa ni maji yanayotoka kuanzia saa 6 usiku hali inayoelezwa kuchangia hali hiyo.


"Maji yanawezaje kutoka saa 6 usiku yashindwe kutoka asubuhi, wakati mwingine unaona wazi kuna mazingira ya hovyo kabisa ya kutaka kuharibu nyumba zetu, tushukuru kwamba kuna mpango wa kuiua CHALIWASA, kisha kutengeneza Mamlaka moja pamoja na DAWASA, maana hawa wameshindwa kuendeleza mradi," alisema Ridhiwani.


Kwa upande wake Diwani Nicholas Muyuwa alisema kuwa halmashauri ya Chalinze inaendelea na juhudi za kupunguza kama si kumaliza changamoto zinazowakabili wana- Ubena, kwa kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya shule, afya na barabara ambazo kwa sasa baadhi yao zinapitika vizuri.


"Niwashukuru wananchi wa Ubena Zomozi kwa ushirikiano na viongozi wao ambao wamekuwa karibu katika kuibua miradi ya kimaendeleo, inayoanzishwa na wenyewe kisha halmashauri na serikali Kuu kuunga mkono juhudi hizo," alisema Muyuwa.


Mmoja wa wakazi aliyejitambulisha kwa jina Idd Mohamed alikiambia kikao hicho kwamba wanakabiliwa na changamoto ya maji, sanjali na mifugo ambayo imekuwa ikiingizwa kwenye mashamba yao hali inayosababisha usumbufu mkubwa.

No comments:

Post a Comment