Monday, May 13, 2019

MBUNGE JUMAA AIKABIDHI POLISI VIFAA VYA MIL. 3

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa ( wa pili kulia) akimkabidhi vifaa hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa, kwa niaba ya Kamanda wa Mkoa, wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Josephine Protas na wa pili kushoto ni
Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa polisi (ASP) Mosi Ndozelo,
 .........................................

Na Omary Mngindo, Kibaha

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, amelikabidhi Jeshi la Polisi Usalama Barabarani mkoani hapa friji ndogo na viti kumi, kwaajili ya kuboresha utendaji kazi dawati la elimu katika jeshi hilo.

Katika hafla fupi ya makabidhiano hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ofisi za jeshi hilo mkoani Pwani, Jumaa amekabidhi friji ndogo na viti kumi kwa Kaimu Kamanda wa jeshi hilo Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa, kwa niaba ya Kamanda wa Mkoa.

Jumaa alisema kuwa, hatua hiyo imefuatia ombi alilopatiwa siku chache na Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa polisi (ASP) Mosi Ndozelo, ambaye alimwelezeea changamoto ya viti na friji, kwa ajili ya matumizi ya ofisi upande wa dawati katika utoaji elimu.

"Nilifika hapa siku mbili zilizopita nikakutana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani hapa, ASP. Mosi Ndozelo, ambaye alinielezea changamoto inayohusiana na utekelezaji wa majukumu ya kazi zao"

Na kufuatia ombi hilo leo nimekabidhi friji ndogo na viti kumi vyenye thamani ya shilingi milioni 3," alisema Jumaa.

Kwa upande wake Kamanda Mwakalukwa alimshukuru Mbunge huyo, huku akitoa rai kwa wadau wengine kuungana katika kusaidia jeshi hilo, ili liweze kuendelea kutimiza majukumu yake kwa ufasaha zaidi.

"Ofisi yetu ina changamoto mbalimbali za vifaa, tunawaomba wadau wajitokeze kutuunga mkono katika kutatua mambo ambayo kwa namna moja au nyingene yanachangia kukwamisha utekelezaji wetu wa majukumu kiufasaha," alisema Kamanda Mwakalukwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Josephine Protas alisema kwamba, kitendo cha Jumaa kujitolea kusaidia jeshi hilo ni cha kuigwa na wabunge wengine, huku akitoa rai kwa wadau wengine kujitokeza katika hilo.

Kamanda wa kikosi cha Usalama barabarani Ndozeli alisema kuwa walimfikishia ombi hilo mbunge huyo siku mbili zilizopita, hivyo ameonesha kujali ombi hilo, hatimae kuwapatia vifaa hivyo.
 
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa ( wa pili kulia) akimkabidhi vifaa hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa, kwa niaba ya Kamanda wa Mkoa.
Picha na Omary Mngindo.

No comments:

Post a Comment