Saturday, May 18, 2019

ULEGA AKABIDHI MIL. 2.5 KUKARABATI ZAHANATI.

Na Omary Mngindo, Mkuranga

MBUNGE wa Jimbo la Mkuranga Mkoa wa Pwani Alhaj Abdallah Ulega, amemkabidhi fundi atayekarabati zahanati ya Kijiji cha Mpafu, Kata ya Dondo Tarafa ya Kisiju kiasi cha sh. Mil 2,560,000 kufuatia kuezuliwa kwa paa lake.


Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Katibu wa mbunge huyo Zuwena Mtuliya alisema kuwa, hatua hiyo inalenga kuirejesha zahanati hiyo katika hali yake ya kawaida, kutokana na kuezuliwa paa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha, iliyoambatana na upepo mkali. 


Akiambatana na diwani wa Kata hiyo Maulid Ubuguyu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata Nassoro Mgalu na Katibu wake Hassani Kiumbo, Mtuliya alimkabidhi fundi Omary Adui kiasi hicho kwa ajili ya ukarabati huo.


"Katika kuhakikisha huduma zinarejea katika hali yake ya kawaida, Mbunge wetu Abdallah Ulega amejitolea kumlipa fundi kiasi cha shilingi milioni 2,560,000 kwa ajili ya ukarabati huo, nimemkabidhi fundi atayefanya kazi hiyo Omary Adui" alisema Mtuliya.


Alisema kuwa kulikuwa na upungufu wa kiasi hicho cha pesa ambazo ni gharama za fundi zilizokwamisha ujenzi huo, ambapo kijiji kilinunua bati za kupaua jengo lote, halmashauri ya wilaya ilinunua mbao, saruji, gypsum, rangi pamoja na misumari.


"Ukarabati unaoendelea kufanyika kwenye zahanati ya Mpafu ni pamoja na kuvunja paa lote, kupandisha ukuta, kupaua, kuvunja sakafu ya awali na kuweka upya, kisha kumalizia kwa kupaka rangi," alisema Mtuliya.


Diwani Ubuguyu alianza kwa kuishukuru halmashauri, mbunge na wananchi kwa juhudi zao ambazo zinaonesha kupatikana kwa mwanga wa kurejesha huduma za matibabu katika zahanati hiyo.

No comments:

Post a Comment