Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania,
Bi. Agnes Mtawa akiwaapisha wauguzi na wakunga kwenye maadhimisho ya Siku ya
Uuguzi na Ukunga Duniani ambayo hufanyika Mei 12, kila mwaka. Leo wauguzi
wameapishwa kukumbushwa kutoa huduma kwa kuzingatia kanuni na taratibu kama
walivyojifunza. Wengine kushoto ni viongozi wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) na viongozi wa Chama cha Uuguzi na Ukunga Tanzania (TANNA)
wakishiriki katika shughuli ya kuwaapisha wauguzi jana Mei 12, 2019.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Bw.
Makwaia Makani akizungumza na wauguzi jana Mei 12, 2109. katika maadhimisho ya siku ya wauguzi
duniani.
...................................
Wauguzi wametakiwa kuendelea kutekeleza majukumu
ya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kitaaluma kwa lengo la kutoa
huduma bora za afya kwa wagonjwa.
Wito huo umetolewa na Msajili wa Baraza la
Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa katika maadhimisho ya siku ya Uuguzi
na Ukunga Duniani ambayo yamefanyika Hopistali ya Taifa Muhimbili (MNH) na
kuudhuriwa na wauguzi na wakunga wa MNH na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI).
Maadhimisho hayo hufanyika Mei 12, kila mwaka na
kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wauguzi Sauti inayoongoza Afya kwa Wote.” Mwaka huu
kitaifa maadhimisho yanafanyika mkoani Katavi.
Bi. Mtawa amewakumbusha wauguzi kuzingatia
mafunzo yanayotolewa mahala pa kazi kwani ndio yanayochochea kutoa huduma bora
ya afya kwa wagonjwa.
Amewataka wauguzi kutambua kwamba huduma
wanayotoa kwa wagonjwa ni huduma ya kibinadamu kwani elimu inachangia kufikia
malengo ya kutoa huduma bora.
“Hivi sasa mambo yetu yanakwenda vizuri.
Malalamiko mengi yamepungua kwani ukifuatilia utabaini kwamba malalamiko mengi
ni ya wagonjwa au mgonjwa kutaka kupewa kipaumbele kupata huduma ya afya badala
ya kufuata utaratibu,” amesema Bi. Mtawa.
Pia, Msajili amewapongeza wauguzi kwa kutekeleza
majukumu ya kutoa huduma za afya kwa kuzingatia taratibu za kitaaluma kwa
asilimia 100.
Akisoma risala katika maadhimishisho, Katibu wa
Chama cha Uuguzi na Ukunga Tanzania, tawi la Muhimbili, Bw. Seif Hamisi ameomba
vitendo vya udhalilishaji kwa wauguzi vifanyiwe kazi kwa kuwa vitendo hivyo
vinawapunguzia ari ya kufanya kazi.
Kupitia risala, Katibu ameishukuru Muhimbili kwa
kuwapatia wauguzi mafunzo mbalimbali ambayo yamewasaidia kutoa huduma bora za
afya kwa wagonjwa.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Bw.
Makwaia Makani amewataka wauguzi kutoa taarifa kwa uongozi wa MNH endapo
watadhalilishwa wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili
watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria.
“Mmesikia jamani nendeni mkawaeleze wenzenu
kwamba endapo muuguzi atadhalilishwa, bila kuchelewa naomba atoe taarifa kwa
uongozi ili wanaofanya hivyo tuwafikishe mbele ya vyombo vya dola,”
amesema Bw. Makani.
No comments:
Post a Comment