Mkuu
wa Wilaya ya Bagamoyo Mheshimwa Zainabu Kawawa amefanya warsha na wadau wa
madini ujenzi, wa halmashauri ya Chalinze katika Ukumbi wa shule ya Sekondari
Lugoba na kuwataka kuzingatia sheria taratibu na kanuni za ulipaji ushuru na
mapato mbalimbali ya halmashauri na kukemea utoaji rushwa ili kukwepa ulipaji
mapato na shuru mbalimbali ambazo zimeainishwa kwa mujibu wa sheria za nchi na
sheria ndogo za halmashauri.
Mkuu wa Wilaya katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha hiyo iliyojumuisha wamiliki wa migodi ya madini ujenzi, kamati ya ulinzi na Usalama na wakuu wa idara wa halmashauri ya Chalinze aliwataka washiriki wa warsha hiyo kuwa waadilifu kwa kuzingatia sheria ya kupambana na kuzuia rushwa namba 11 ya mwaka 2007 na sheria zingine za nchi zinazohusu mapambano dhidi ya rushwa.
Naye Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Bagamoyo Bwana Raymond Katima alitoa mada ya mapambano dhidi ya rushwa kwa washiriki wa warsha na kuwataka kuzingatia sheria za nchi, pia aliweza kutoa taarifa fupi ya uchunguzi wa namna ya ukusanyaji mapato katika halmashauri ya Chalinze kwa upande wa madini ujenzi na kueleza kuwa mapato yanayotokana na madini kokoto hayakusanywi inavyotakiwa kwani kuna ukwepaji kwa namna moja au nyingine kwa wamiliki wa migodi.
Katima
alieleza madhara ya rushwa kwa maendeleo ya nchi na kuwaagiza washiriki katika
makampuni yao kuendelea kutoa Elimu ya mapambano dhidi ya rushwa mara kwa mara
kwani rushwa ni suala mtambuka ambalo linatakiwa kuzungumziwa kila wakati
mahali pa kazi.
Kamanda wa TAKUKURU aliwasilisha changamoto za kiutendaji katika ukusanyaji wa Mapato na mapendekezo ya utatuzi wa changamoto hizo ili ukusanyaji wa Mapato ya serikali uweze kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na kwa ufanisi zaidi.
Mapendekezo yaliyotolewa katika warsha hiyo ni pamoja na kuweka waangalizi watakaokuwa wanashuhudia namna kokoto zinavyotoka kutoka eneo la uzalishaji kwenda kwa watumiaji, waangalizi hao watakuwa kila sehemu patakapokuwa na uzalishaji wa kokoto ili kudhibiti upotevu wa mapato ya halmashauri. Sanjari na hilo washiriki katika warsha hiyo walikiagiza kitengo cha Tehama kuzikagua mara kwa mara mashine za kukusanyia mapato ili zisihujumiwe na kutumika vibaya na watu wasio waadilifu.
Mheshimiwa Kawawa alimalizia hotuba yake kwa kuwataka wamiliki wa makampuni kuwa wazalendo kwa kulipa kodi na shuru mbalimbali kwa wakati pasipo shuruti na kuendelea kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano kwa kutoa huduma bora kwa wananchi katika halmashauri ya Chalinze.
No comments:
Post a Comment