Monday, May 6, 2019

WAGANGA WAKUU WA MIKOA WAPEWA MWEZI MMOJA KUTATHMINI UTENDAJI WA KAMATI ZA AFYA ZA MIKOA NA WILAYA ZAO.

 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia afya Dkt Dorothy Gwajima akizungumza na Kamati ya uendeshaji ya huduma za afya ya mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
..........................................


Waganga wakuu wa Mikoa Tanzania Bara wamepewa mwezi mmoja kuhakikisha kuwa wanazifanyia tathmini ya kina Kamati za Uendeshaji Huduma za Afya za Mikoa na Wilaya zao kuona kama zinaendana na kasi ya mabadiliko yanayokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Tano.


Agizo hilo limetolewa jana Mei 05, 2019  mjini Songea na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji Huduma za Afya ya Mkoa wa Ruvuma pamoja na Wajumbe wa Kamati za Uendeshaji Huduma za Afya kutoka Halmashauri ya Namtumbo, Halmashauri ya Wilaya ya Songea pamoja na Manispaa ya Songea.


Alisema anawapa siku 30 Waganga Wakuu wa Mikoa yote kuhakikisha kuwa wanafanya tathmini ya Wajumbe waliopo katika ofisi zao kama wanatosha kuendelea na nyadhifa zao za kusimamia jukumu la uendeshaji huduma za afya katika mikoa na halmashauri zao.


Dkt Gwajima ameongeza kuwa endapo itabainika kuwa baadhi ya Wajumbe wa Kamati hizo hawana sifa na kupelekea kushindwa kutekeleza majukumu yao ya usimamizi na uendeshaji huduma za afya katika maeneo yao, Waganga Wakuu wa Mikoa watalazimika kuwaweka pembeni Wajumbe hao na kuunda upya Kamati ambazo zitaweza kuiendeleza agenda ya mabadiliko katika sekta ya afya.


“Kinyume na hapo katika ziara hizi ninazoendelea kuzifanya mikoani nikikuta yupo Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye ametulia tu, mapungufu katika vituo bado yapo na amewezeshwa na Serikali, ajue wazi kuwa yeye atakuwa kuwa hatoshi” alisema Dkt Gwajima na kuongeza:


“Haiwezekani tukute mapungufu madogo kabisa katika vituo, ambayo yangeweza kuonwa na wao walioko huko eti hayaonekani hadi tuje sisi kutoka Tamisemi ndiyo mapungufu hao yafanyiwe kazi,”amesisitiza Dkt Gwajima.


Naibu Katibu Mkuu huyo ameonya tabia iliyojengeka miongoni mwa Wajumbe wa Kamati za Uendeshaji Huduma ya Afya kukimbilia kuomba msamaha pindi zinaposhindwa kutekeleza majukumu yake kwa makusudi.


Alisema huu ni wakati wa kuboresha sekta ya afya katika vituo vya afya na zahanati kwa kuhakikisha kuwa mazingira ya utoaji huduma yanaboreshwa ili yaweze kuwavutia wananchi wengi kukimbilia kupata huduma katika zahanati na vituo vya afya vinavyomilikiwa na serikali ikiwemo hospitali za halmashauri.


Dkt Gwajima amesema kuwa kamwe hatawapa nafasi Wajumbe wa Kamati za Uendeshaji Huduma za Afya wa Mikoa na Wilaya ambao siku zote wamekuwa ni watu wa visingizio vya kuomba kusamehewa ama kupewa muda kuwa wamefahamu mapungufu yao wakati mapungufu husika ni yale yale ambayo kila siku Serikali inatoa maelekezo kuwa yafanyiwe kazi.


Alisema angependa kuona Kamati za Uendeshaji Huduma za Afya katika Mikoa na Halmashauri zikijikita katika kuongelea mambo ya ubora wa huduma kwa mteja “’quality care” na kuwa, mteja ni mfalme na si vinginevyo. 

Serikali imeshirikisha Wananchi na kutuwezesha miundombinu safi na dawa za kutosha, bajeti ya kufuatilia huduma inatolewa, semina za uongozi zinafanyika, maelekezo yanatolewa je, tatizo huwa linatokea wapi?


“Hivi vitu vidogo vidogo vya kitaalamu tubebe sisi wenyewe, Wananchi wametuunga mkono, tumeweza kushirikiana nao kujenga zahanati na vituo vya afya katika mikoa na halmashauri zetu hivyo ni jukumu letu sasa kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bora za afya kwa Wananchi na kuondoa hii tabia ya kuwepo kwa malalamiko yanayosababishwa na uzembe katika kufuatilia na kusimamia,” alisema.


Kwa mujibu wa Dkt. Gwajima, katika ziara zake alizokwisha zifanya katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Njombe na Songea amejionea mapungufu mbalimbali ya utoaji wa huduma bora za afya katika vituo vya afya na zahanati ambayo yapo ndani ya uwezo wa Kamati za Usimamizi na Uendeshaji Huduma za Afya katika mikoa na halmashauri husika.


Ameongeza kuwa mapungufu hayo ambayo ameyashuhudia kwenye vituo vya afya na zahanati zinazomilikiwa na umma yametokana na watoa huduma waliopo katika vituo hivyo kutopata usimamizi unaostahili kutoka kwa Kamati za Usimamizi na Uendeshaji wa Huduma za Afya za Mikoa na Halmashauri husika.


Dkt Gwajima anaamini kuwa, kushindwa kwa Kamati za Uendeshaji na Usimamizi wa utoaji huduma za afya katika ngazi za mikoa na halmashauri kutekeleza majukumu yao, ndiko kulikopelekea kukithiri kwa uchafu katika majengo ya vituo vya afya na zahanati, kushindwa kufanyiwa matengenezo muhimu ya kuboresha mazingira ya zahanati na vituo hivyo licha ya vituo hivyo kuwa na fedha za uendeshaji wake.


 “Unakuta kituo kina fedha za kutosha kwenye akaunti lakini mapungufu madogo madogo ya kukera yamejaa,” ameeleza Naibu Katibu Mkuu.


Amesema hali hiyo imesababishwa na kushindwa kwa Kamati za Uendeshaji Huduma za Afya za Mkoa (RHMT) na zile za Halmashauri (CHMT) kwa kutofanya kazi ya ufuatiliaji wa utoaji huduma bora na utaalam kwenye vituo vya afya nchini licha ya kuwezeshwa na Serikali.


Sambamba na kuwataka Waganga Wakuu wa Mikoa kuzitathmini Kamati hizo, Dkt Gwajima pia amewataka wajumbe wa Kamati hizo kutambua kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ipo na agenda moja tu ya kuleta mabadiliko katika sekta ya afya na kuwagusa watumiaji wa huduma hizo kwa huduma zenye ubora unaostahili.


“Hatutapimwa kwa idadi ya semina au uwepo wa kituo cha afya tu karibu na Wananchi bali kwa ubora huduma zinazotoleewa katika vituo hivi, vinginevyo Wananchi watakuwa karibu na vituo husika lakini hawavitumii,” amesema.


Dkt Gwajima amebainisha mapungufu kadhaa aliyoyaona kwenye ziara yake kuwa ni pamoja na Kamati za Uendeshaji Huduma ya Afya kushindwa kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye vituo vyao vya afya na zahanati, kuwepo kwa malalamiko toka kwa wagonjwa, kukosekana kwa takwimu sahihi za utendaji kazi na Wajumbe wa Kamati za uendeshaji huduma za Afya kushindwa kuandika vizuri kumbukumbu za taarifa za kazi za ikiwemo mihutasari ya vikao na wengine kutokaa kabisa vikao muhimu.


Akiwa katika kituo cha afya Mjimwema Manispaa ya Songea Naibu Katibu Mkuu Dkt.Gwajima alipokea kero za wagonjwa kuhusu uwepo wa kauli mbaya toka kwa baadhi ya watumishi wakiwemo wauguzi na matabibu, tatizo la ukosefu dawa na vifaa tiba muhimu hususan vya akina mama wajawazito.


“Hapa Mjimwema nimebaini kasoro nyingi mojawapo kauli mbaya za watumishi na tatizo la dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa ” ameonya Dkt .Gwajima.


Aidha, alimpongeza tabibu msaidizi mmoja aliyeibuliwa na mteja kwamba, anatamani watoa huduma wote wangekuwa kama tabibu huyo anayeitwa Lidya Mwakyusa Hii ni mara ya pili kwa wateja kuwataja hadharani watumishi watoa huduma wenye huduma inayojali mteja akiwemo Edward Mapunda wa Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Njombe.


Dkt. Gwajima amewapongeza watoa huduma wanaotambua wajibu wao kuwa, mteja ni mfalme na amewataka kutovunjwa moyo na baadhi ya watumishi wasiozingatia maadili ya kazi na kuleta kero kwa wateja.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Jairy Khanga ameahidi kuchukua hatua za mapema kufanya mabadiliko ya utendaji kazi wa Kamati za Usimamizi wa Huduma za Afya katika Mkoa wa Ruvuma

 

No comments:

Post a Comment