Monday, May 13, 2019

TASAF LINDI WABUNI MRADI WA KUPANDA MIKOROSHO KUNUSURU KAYA MASKINI.

NA HADIJA HASSAN 12/05/2019 LINDI.

Wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi wamefanikiwa kupanda Miche 3,039 ya Mikorosho katika mashamba yenye ukubwa wa hekari 121 na kufanikiwa kujipatia ujira wa Tsh. Milioni 437.6

Hayo yameelezwa na Mratibu wa TASAF wa manispaa hiyo Dativa kysima alipokuwa anatoa taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika Halmashauri yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi Mwishoni mwa wiki alipokwenda kutembelea pamoja na kuzungumza na walengwa wa Mpango huo katika halmashauri hiyo.

Kysima alisema walengwa hao ni wale ambao wanatekeleza mradi huo kupitia mpango wa ajira za muda mfupi.

Aidha Kysima aiitaja mitaa iliyotekeleza mradi huo wa kupanda miche ya Mikorosho kuwa ni Mitumbati ambapo wamefanikiwa kupanda miche 45 katika shamba lenye ukubwa wa hekta 2 na kufanikiwa kupata ujira wa Tsh. 10.777,800.00, mtaa wa kiduni ambapo umepanda miche 208 katika shamba lenye ukubwa wa hekta 8 na kupata ujira wa kiasi cha Tsh.10,959,500, mtaa wa Chikonji Kaskazini miche 307 kwa shamba lenye ukubwa wa hekta 12 na kupata ujira wa 23,740.600 na mtaa wa Chikonji Kusini miche 307 kwa shamba lenye ukubwa wa hekta12 na kupata ujira wa Tsh.12,045,100

Aliitaja mitaa mingineni kuwa ni Mtaa wa Kikwetu ambao umepanda miche 333 katika shamba lenye ukubwa wa hekta 13 na kupata ujira wa Tsh.5,448,700, 00, mtaa wa Mingoyo miche 122 katika shamba lenye hekta 5 huku wakipata ujira wa Tsh.18,018,200,00, mtaa wa Mawasiliano ambao umepanda Miti 178 katika shamba lenye ukubwa wa Hekta 7 na kupata ujira wa Tsh.14,524,500,00.

Mitaa mingine iliyotekeleza mradi huo ni Nanyanje ambao wao wamepanda miche 320 katika shamba lenye ukubwa wa Hekta 13 na kupata ujira wa Tsh.8,429,500.00, Mtaa wa Jangwani miche 120 katika shamba lenye ukubwa wa Hekta 5 na kupata ujira wa fedha ya Tsh.13,298,600.00 na mwisho ni Mtaa wa ambao umepanda miche 1100 katika shamba lenye ukubwa wa Hekta 44 na kupata ujira wa Tsh. 20,382,600.00

Awali Mkurugenzi wa Manspaa ya Lindi Jomary Satura alisema kuwa kabla ya kubuni mradi huo wa mashamba wanufaika hao wa TASSAF ambao wanatekeleza mradi wa ajira za muda walikuwa wanawatumia katika kufanya usafi kwenye maeneo yao ya mitaa pamoja na meneo ya Umma kama vile maeneo ya sokoni , katika hospitali na zahanati pamoja na stendi

“walikuwa wanafanya shughuli hizo na baadae tunawalipa lakini tukaona hiyo sio sawa kwa kuwa shughuli zile tulikuwa tunapaswa kufanya wenyewe kama Halmashauri ndipo tukabuni huu mradi wa mashamba ya mikorosho ambapo tulikubaliana na wanufaika hawa kufanya usafi katika mashamba hayo pasipo kuwaambia kuwa baadae mashamba hayo yatakuwa yakwao” alisema Satura.

Satura aliongeza kuwa Baada ya mashamba hayo kufanyiwa usafi pamoja na kupanda miche ya Mikorosho sasa yatakuwa yanamilikiwa na wanajamii wa maeneo husika ambao wamekuwa katika mpango huo wa kunusuru kaya maskini

Nae mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga alisema kuwa Lengo kuu la mpango huo ni kuwafanya wanufaika hao kuondokana na umasikini Alisema ni wazi kuwa baada ya miaka kadhaa mikorosho hiyo itakapoanza kuzalisha wananchi hao hawatakuwa maskini tena

Akizungumza na wanufaika hao wa Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii TASSAF Mkuu wa Mkoa wa Lindi aliupongeza uongozi wa Halmashauri hiyo kwa mawazo mazuri ya kuanzisha kitega uchumi kikubwa ambacho kitakwenda kuwasaidia wananchi hao katika kujiongezea kipato pamoja na kuwapongeza wanufaika hao kuupokea mradi huo na kuutekeleza

Zambi alisema ni muhimu kwa halmashauri zote za mkoa huo kuiga mfano uliofanywa na Halmashauri hiyo huku akimuagiza katibu Tawala kuwaandikia Barua Wakurugenzi hao juu ya kutekeleza jambo hilo

Zambi alisema ifike mahala sasa fedha hizo zinazotolewa na Serikali ziwe zinaleta tija kwa wanufaika ikiwa pamoja na kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuinua uchumi wa wanajamii ambao wamekuwa katika Mpango huo.

No comments:

Post a Comment