Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kulia ) akipokea maelezo
kutoka kwa mmoja wa wakunga ya namna wanavyowahudumia wakina mama wajawazito na
watoto wakati alipotembelea Banda la Chama cha Wakunga Tanzania(TAMA),
katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika
Uwanja wa Bariadi Mkoani Simiyu.
......................................
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ametoa rai kwa
viongozi wa Kisiasa hapa nchini kuacha kuingilia kazi za Kitaaluma katika sekta
ya Afya na kuwaomba wawaache wataalam wafanye kazi zao kwa misingi na miiko ya
Kitaaluma inayowaongoza.
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo katika
Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa
Halmashauri ya Mji wa Bariadi, chini ya Kauli Mbiu “Wakunga Watetezi wa Haki za
Wanawake”, ambapo alikuwa akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Amesema hivi karibuni kumekuwa na
matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa yanayowakatisha tamaa
watumishi wa sekta ya afya na baadhi ya viongozi wameanza kuingilia masuala ya
kitaalum, hivyo akawaomba ikiwa viongozi hao watakutana na changamoto za
watendaji wa afya waishirikishe wizara ya afya ili wachukuliwe hatua kwa
mujibu wa taaluma zao.
“Niwaombe sana viongozi wa Serikali
na Viongozi wa vyama, masuala ya kitaaluma yanashughulikiwa kitaaluma kama kuna
changamoto na wanataaluma ndiyo maana tuna mabaraza ya taaluma na ndiyo maana
sisi wizara tupo mtushirikishe, nimelisema hili kwa sababu nimeona sekta
imeanza kuingiliwa” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha, Dkt. Faustine Ndugulile
amewataka wakunga hapa nchini kuendelea kuzingatia miiko na misingi ya taaluma
yao katika huduma wanazotoa kwa jamii na kuahidi kuwa Serikali haitasita
kuwachukulia hatua wale wote watakaokiuka misingi hiyo kwa kuwa jamii inahitaji
heshimu, utu, upendo na kutiwa moyo
Katika hatua nyingine.
Dkt. Ndugulile
ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na jamii kwa ujumla
kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya ili
changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi vibaki kuwa historia ambapo amesema kwa
sasa wanawake 11,000 wanakufa kila mwaka kutokana na uzazi.
Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania,
Bibi. Feddy Mwanga ameiomba Serikali kuongeza idadi ya wakunga ili mkunga aweze
kutoa huduma kwa kiwango kinachokubalika Kitaifa na kimataifa huku akisisitiza Serikali
kuona haja ya kujenga nyumba za wakunga katika vituo vyote vya kutolea huduma
za afya vinavyoboreshwa na vinavyojengwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.
Festo Kiswaga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthoy Mtaka
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kutoa shilingi bilioni saba fedha kwa ajili ya ujenzi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa
Hospitali tatu za Wilaya Bariadi, Busega na Itilima ambazo ujenzi wake
unaendelea vizuri.
Aidha, Kiswaga ameshukuru Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani(UNPFA) kwa namna
linavyoshirikiana na Serikali mkoani Smiyu kwa kukarabati baadhi ya vituo,
kununuaa vifaa mbalimmbali, kutoa mafunzo kwa wakunga jitihada ambazo
zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Akitoa taarifa ya Mkoa, Katibu Tawala
wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema
Idadi ya wakunga katika vituo vya
kutolea huduma za afya Simiyu imeongezeka hali iliyofanya wajawazito wengi
kujifungulia katika vituo vya afya kutoka asilimia 62 mpaka asilimia 68, hivyo
vifo vya mama wajawazito vimepungua kutoka vifo 48 mwaka 2017 mpaka vifo 40
mwaka 2018.
Naye Makamu Mwakilishi Mkaazi wa
UNFPA hapa nchini, Dkt.Hashina Begum amesema kwa kushirikiana na Chama cha
Wakunga nchini (TAMA) limetoa mafunzo kwa wakunga 90 kutoka katika vituo
vilivyoboreshwa ili kuwasaidia wakina mama wajawazito na watoto kupata huduma
za dharura na kupunguza vifo kwa mama na mtoto vitokanavyo na
uzazi.
Grace Magengeni Mkunga kutoka Jijini
Dodoma amesema” siku yetu imefana tunashukuru hotuba ya Naibu Waziri imetutia
moyo katika kuwahudumia wanawake na watoto, nawashauri wenzangu tusimamie
taaluma zetu tufanye kazi kwa bidii naamini hao wanaotuingilia majukumu yetu
wataachaa maana ni kweli, tunashukuru Naibu Waziri kulisemea hili suala”
No comments:
Post a Comment