Idara ya Afya katika Halmashauri ya
Wilaya ya Bagamoyo, imeendesha zoezi maalum la utoaji dawa kinga kwa ajili ya
kinga tiba ya kichocho na minyoo tumbo, kwa watoto wenye umri kati ya miaka 5 –
14.
Zoezi hilo limezinduliwa jana katika
Uwanja wa Shule ya Msingi Kizuiani iliyopo kata ya Kisutu, ambapo Mgeni rasmi
Dkt. Salvio Wikesi aliyemwakilisha Mkuu ya Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainab
Kawawa, amewatoa hofu Wananchi, hususani Wazazi juu ya utoaji wa dawa hizo,
akisisitiza kwamba, dawa hizo ni kinga tiba na si
chanjo kama inavyofahamika na wengi, na akaongeza kuwa dawa hizo ni salama na
zimethibitishwa ubora wake na mamlaka zinazohuzika.
“Kumekuwa na dhana potofu kwenye
jamii, kuwa dawa hizi si salama, hivyo wazazi kukataa watoto wao wasipewe dawa
hizi na wakati mwingine kuwakataza watoto wasifike Shuleni siku ambazo dawa
zinatolewa.
Nachukua fursa hii kuwaondoa hofu wazazi na Wananchi wote kuwa dawa
hizi ni salama na muhimu kwa watoto wetu na wawaruhusu watoto kupatiwa dawa
kinga hizi, kwani magonjwa haya yasiyopewa kipaumbele ni hatari na yaweza hata
kuhatarisha uhai wa mtoto anapochelewa kupatiwa matibabu yake” Amesema Dkt.
Wikesi.
Nae Mratibu wa Kitengo cha Magonjwa
yasiyopewa kipaumbele kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Ndg. Mohamed Farah
amesema lengo la utoaji wa dawa kinga hizo Mashuleni ni kutoa kinga na tiba kwa
magonjwa ya kichocho na minyoo tumbo kwa Watoto wote wenye umri wa miaka 05-14
waliopo Shuleni na nje ya Shule (nyumbani).
Akaongeza, kwa Mwaka 2018, zoezi hili
la utoaji dawa kinga kwa watoto wenye umri wa miaka 05-14 lilifanikiwa kwa
90.2/% na kwa Mwaka huu wanatarajia kupata mafanikio zaidi kwani wamefanya
uhamasishaji wa kutosha kwa jamii na kusisitiza kuwa kwa watoto ambao hawako
Shuleni, wazazi wawapeleke watoto hao katika vituo vya Afya, Zahanati na
Hospitali ili kupatiwa dawa hizo.
Zoezi hili la utoaji dawa za Minyoo
tumbo na Kichocho pia linaendelea katika Vituo vyote vya Afya, Zahanati na
Hospitali ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.
imeandaliwa na Afisa habari Halmashauri ya Bagamoyo
No comments:
Post a Comment