Wednesday, May 22, 2019

RIDHIWANI KIKIKWETE ATOA NENO KWA WA ISLAM.

 
 Na Shushu Joel, Chalinze.

MBUNGE wa jimbo la chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete amewataka waislamu kutumia nafasi hii katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kuwaombea viongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri na kuleta maendeleo kwa jamii yote hapa nchini.

Rai hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu katika Kata ya Pera kitongoji cha Magome alipokuwa akikabidhi Msikiti wa Masjid Swafiya uliojengwa kwa msaada wa Mbunge huyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Miraji Islamic Center.

"Kipindi kama hiki cha mfungo tunatakiwa kumcha Mwenyezimungu na kusaidia masikini kwani funga inamaana kubwa sana hapa duniani hivyo kila mwislamu aliyefanikiwa kupata nafasi hapa duniani ni lazima amsaidie mwenzake japo futali" alisema Kikwete.

Alisisitiza kuwa mwezi huu wa Ramadhani ni mwezi ambao tunasisitizwa kusoma sana Qur'an kwasababu ndio mwezi ambao Qur'an iliteremshwa kupitia kwa Mtume Muhammad Swalla llaahu Alayhi Wasalaam ili uwe muongozo kwa watu wote hapa duniani, pia usomaji huo unamalipo makubwa sana kwa Mungu.

Aliongeza kuwa kutokana na jinsi viongozi wa Serikali wanavyopambana kufanikisha maendeleo kwa wananchi wanyonge kwa kubana wenye kutumia raslimali za wananchi vibaya ni lazima viongozi hao wachukiwe na baadhi ya watu.

Aidha mbunge huyo amempongeza Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa juhudi zake anazozifanya katika utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (ccm) kwa ufanikishaji wa maendeleo kwa wananchi wanyonge.

Kwa upande wake Shehe Mohamed amempongeza Mbunge huyo kwa kutambua thamani ya uislamu na hata kujitolea kwa hali na mali katika ufanikishaji wake wa ujenzi wa msikiti huo katika Kata ya pera.

Hivyo amemuhakikishia Kikwete kuwa wao kama viongozi wa dini wataendelea kuliombea Taifa hili ili liondokane na majanga ya aina yeyote ile na wananchi wake kuweza kunufaika zaidi na maombezi ya viongozi wao wa dini.

Naye Tatu Mkenge amemshukuru Mbunge wa jimbo hilo katika dhamira yake ya kupambania ujenzi wa msikiti wa Magome ili kuwaondolea changamoto ya mahali pa kumuomba Mwenyezimungu.

Aidha amewataka waislamu kote kuongeza juhudi za kuwaombea viongozi mbalimbali ili utendaji wao wa kazi uendelee kutukuka na uwe wenye kumuogopa Mungu.

No comments:

Post a Comment