Monday, May 6, 2019

KIZIMBANI KWA KUBAKA MTOTO CHINI YA MIAKA 10.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

MKULIMA wa Kijiji na Kata ya Rutamba, Halmashauri ya Wilaya Lindi Mkoa wa Lindi, Issa Seif Puyaye (51) amefikishwa mahakamani akikabiliwa na Shitaka la kubaka Mtoto mwenye umri chini ya miaka kumi (Jina linahifadhiwa).


Puyaye amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Lindi na kusomewa Shitaka lake mbele ya Hakimu Faudhia Jemedari, na mwanasheria wa Serikali Godfrey Mramba. 


Akimsomea Shitaka lake, Mramba alidai kuwa Aprili 14 mwaka huu, Mshitakiwa alikamatwa na askari wa Jeshi la Polisi, kufuatia wazazi wa Mtoto huyo kutoa taarifa kwenye chombo hicho. 


Mramba alidai Mahakamani hapo kuwa wazazi wa Mtoto huyo anayesoma Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Mpilipili iliyopo Manispaa ya Lindi,walichukuwa uwamuzi huo baada ya kupewa taarifa na walipomkagua waliweza kubaini kufanyiwa kitendo hicho cha kinyama. 


Alidai kwamba kutokana na kitendo hicho mshitakiwa amefanya kosa kwa mujibu wa kifungu 130 (1) (2) (e) na 131 (1) Sheria na kanuni ya adhabu ya makosa sura ya 16/2002. 


Mwanasheria huyo aliiambia Mahakama hiyo kwamba mshiatkiwa alipata nafasi ya kumfanyia unyama huo, kutokana na Mtoto huyo kwenda likizo kwa ndugu zake wengine. 


Hata hivyo mshitakiwa amekana kosa na kesi hiyo namba 34/2019, imepangwa kusikilizwa tena Mahakamani hapo Mei 13 mwaka huu, na mshitakiwa amepelekwa rumande baada ya kukosa wadhamni.


No comments:

Post a Comment