Monday, May 20, 2019

SERIKALI KUHAMASISHA UFUGAJI NYUKI

Serikali ya Tanzania imesema ipo mbioni kuja na mpango mkakati wa kitaifa wa kutoa hamasa kwa wananchi kutambua umuhimu wa kufuga nyuki na faida ya asali kiuchumi na kiafya.


Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 20, 2019 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla katika maadhimisho ya siku ya nyuki duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dodoma.


Dk Kigwangalla amesema lengo ni kuwasaidia wananchi wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki kuchakata na kusindika asali kwa pamoja ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.


“Lengo la kuanzisha mpango huo wa kitaifa ni kuwaenzi nyuki kwa kuwekeza fedha ya Serikali na ujuzi kutoka kwa wataalam. Kwa wananchi ni kuunda ushirika kwa mikoa kumi ya Tanzania Bara, na kila wilaya kuwapa mizinga ambayo wataitumia kwa ajili kufuga nyuki,” amesema Dk Kigwangalla.


Amebainisha kuwa baada ya hapo kila wilaya itakuwa na ushirika na kiwanda kimoja kitakachokuwa kinachakata na kusindika asali.

No comments:

Post a Comment