Na
Omary Mngindo, Mlandizi.
MKURUGENZI
wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani Butamo Ndalahwa, amewaahidi
gari viongozi na wachezaji wa timu ya soka ya Mlandizi Queens, inayoshiriki
Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara.
Ndalahwa ametoa ahadi hiyo mwishoni mwa
wiki, alipotembelea kambi ya timu hiyo iliyopo Mlandizi Kibaha Vijijini mkoani
hapa, ambapo alisema ameguswa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa
gari inayoikabili timu hiyo.
Alisema kuwa mara kadhaa viongozi na wachezaji wa
timu hiyo wamefika ofisi kwake, wakihitaji mchango kwa ajili ya kukodi basi
litakalowapeleka mikoani kwa ajili ya ushiriki wa michuano ya Ligi wanayoshiriki
inayoendelea ukingoni.
"Muda mfupi nilikuwa na wachezaji wenzenu na
kiongozi katika upandaji wa miti kwenye hospitali yetu inayojengwa Disunyara,
tukiwa pale nilizungumza na Mbunge Humoud Jumaa kuhusiana na changamoto ya usafiri
inayowakabili," alisema Butamo.
Aliongeza kwamba binafsi amepokea
changamoto ya usafiri inayowakabili, huku akiahidi kulifikisha suala hilo ngazi
ya Mkoa, ambapo alisema anaimani watashirikishwa wabunge kuhakikisha timu hiyo
inakuwa na usafuri wake.
"Historia yangu ni mwanamichezo, kwakuwa mpo
katika halmashauri yetu nitahakikisha nafanya juhudi za kupatikana kwa gari la
timu yatu, Rais wetu John Magufuli ameonesha njia katika michezo hivyo nasi
hatuna budi kuunga mkono juhudi hizo," alisema Ndalahwa.
Kwa upande wake
nahodha wa timu hiyo Wema Richard alimshukuru Mkurugenzi huyo, huku akisema
kwamba wanakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ya kutoungwa mkono na
mashabiki hali inayosababisha kujiona kama wakiwa.
Kiongozi wa timu hiyo Miraji
Miraji alifurahia ahadi hiyo, huku akisema kwamba kwa sasa wachezaji wanadai
posho kiasi cha shilingi milioni moja, ambapo Butamo ameahidi kuwapatia, huku
akianza na shilingi laki tano atayoikabidhi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment