Sunday, May 26, 2019

RIDHIWANI NA MIRAJI FOUNDATION WAGAWA FUTARI

Katibu wa Mbunge Jimbo la Chalinze, Iddi Swala (kulia) akikabidhi futari kwa wakazi wa cha Magome kata ya Pera Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, futari imetolewa na Taasisi ya Miraji Foundation.
............................................
 
Na Omary Mngindo, Chalinze

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Ridhiwani Kikwete, akishirikiana na Taasisi ya Miraji Foundation wamegawa futari kwa waumini wa dini ya Kiislamu Msikiti wa Swafiyyah uliopo Kitongoji cha Magome kata ya Pera jimboni humo.


Katika hafla hiyo fupi iliyofanyika msikitini hapo, Idd Swala Katibu wa Mbunge ndiye aliyakabidhi kwa niaba ya Mbunge Ridhiwani Kikwete, huku Abdilah Makuluta akiiongoza Taasisi ya Miraji ambayo ni rafiki wa mbunge kwa kusaidia kwenye nyanja mbalimbali za kijamii.


Akizungumza kabla ya ugawaji futari hiyo ambayo ilikuwa na ujazo wa tani moja ya, Makuluta alisema kuwa Taasisi yao chini udhamini wa Muft Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zuber ikiongozwa na Mkurugenzi Halifa Abdurahamaan, imejiwekea utaratibu wa kugawa futari kila mwaka kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


"Kwaniaba ya uongozi wa Miraji Foundation chini ya udhamini wa Muft Sheikh Mkuu Aboubakar Zuber ikiongozwa na Mkurugenzi Halifa Abdulhaman, tumekuwa na utaratibu wa kugawa futari kila mwaka kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, leo tupo hapa Magome Kata ya Pera halmashauri ya Chalinze," alisema Makuluta.


Kwa upande wake Iddi Swala akizungumza kwa niaba ya Mbunge, alianza kuishukuru taasisi hiyo kwa misaada mbalimbali  inayotoa jimboni humo, huku akieleza kwamba Msikiti wa Swafiyyah uliopo kitongojini hapo pia umejengwa na taasisi hiyo.


"Ndugu zetu wa Miraj Foundation wamekuwa karibu nasi kusaidia maendeleo ya jimbo letu katika nyanja mbalimbali, huu msikiti tunaofanyia shughuli hii fupi leo, wameujenga wao, tuendelee kuwaombea Mwenyezimungu awazidishie kila la kheri, ili mwakani inshaaAllaah watuletee zaidi ya hiki tulichokipata" alisema Swala, katibu wa Mbunge wa Chalinze.


Kwa upande wake Tatu Mkenge kwa niaba ya wana-Magome alianza kumshukuru mbunge Ridhiwani Kikwete na washirika wake, kwa kuona umuhimu wa kuwafikia katika kuwaunga mkono kwenye mfungo huo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Idd Mbato aliishukuru taasissi hiyo na mbunge Ridhiwani, huku akimuomba mbunge aendelee kuwatafutia wahisani wengine wasaidie nyanja nyingine ndani ya Kitongoji chake na Kata kwa ujumla.
 
Katibu wa Mbunge Jimbo la Chalinze, Iddi Swala akikabidhi futari kwa Mgaza Makunja, mkazi wa cha Magome kata ya Pera Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, futari imetolewa na Taasisi ya Miraji Foundation.
 
 Katibu wa Mbunge Jimbo la Chalinze, Iddi Swala akikabidhi futari kwa mkazi wa cha Magome kata ya Pera Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, futari imetolewa na Taasisi ya Miraji Foundation.

Picha zote na Omary Mngindo.
  

No comments:

Post a Comment