NA
HADIJA HASSAN, LINDI.
KIZITO
Mathey Mgogo (59) Mkazi wa Kata ya Rutamba, Halmashauri ya Wilaya ya Lindi
Mkoani Lindi amelazwa katika Hospitali ya Mkoa huo, Sokoine, akiugulia majeraha
aliyoyapata baada ya kushambuliwa na Simba nyakati za usiku.
Hayo
yameelezwa na mdogo wake Michael Mathei alipokuwa akizungumza na BAGAMOYO KWANZA
BLOG Jana Mei 05, 2019, ilipotembelea Hospitalini hapo.
Michael
akizungumzia mkasa huo, alisema kaka yake anayekabiliwa na tatizo la akili, alipatwa
na mkasa huo Aprili 26/2019, kati ya Saa 5:00 na 6:00 usiku akiwa amejilaza
kwenye Kibanda kinachotumiwa na wajasiliamali wadogo wa kuuza Chakula.
Alisema
siku hiyo Kizito akiwa anarejea Nyumbani kutoka katika mihangaiko yake, alipofika
eneo la Namatili ndipo alikuta Kibanda hicho, kilichokuwa kimejengwa kwa
kuzungushia Fito maeneo ya Pembeni bila ya kukandikwa kwa udogo, aliamua
kuingia na kujilaza.
Michael
aliendelea kuseama kuwa, kaka yake akiwa
kwenye usingizi Simba wawili waliokuwa
kwenye mawindo yao, waalikuwa wakikimbiza Mbwa waliokuwa maeneo ya Simba hao
bila mafanikio, na walifika Kibandani hapo wakasimama na kuangalia kilicho
ndani.
Alisema
baada ya Simba hao kubaini ndani ya Kibanda kile kuna kitu na kukosa eneo la
kupita, ndipo mmoja wa wao aliamua kupitisha mkono wake kupitia matundu ya
Fito, ambapo kucha za Simba huyo zilifikia kati ya tumbo na Kifua cha Kaka
yake, ambae alishtuka na kupiga kelele kuashiria kuomba msaada kutoka kwa
majirani.
Michael
alisema kutokana na kelele hizo Simba wale waliamua kuondoka huku wakimuacha
Kizito akiendelea kuvuja Damu zilizotokana na kubanwa kucha za mnyama huyo.
Alisema
wasamalia walipofika eneo la Kibanda hicho walimkuta tayari ameshajeruhiwa
ambapo walimchukuwa hadi Kituo kidogo cha Polisi Kata ya Rutamba na kupatiwa
Fomu namba tatu (PF3) na kumkimbiza Kituo cha Afya cha Rondo.
Hata
hivyo kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Mganga wa Kituo hicho aliamuru
apelekwe Hospitali ya Sokoine kwaajili ya matibabu.
Mmoja
wa watumishi wa Hospitali hiyo, Dkt. Ernest Muhando, amesema wamempokea
Majeruhi Kizito akiwa na majeraha kati ya kifua na tumboni, yaliyosababishwa na
kushambuliwa na kucha za Simba.
Alisema
mara baada ya kufikishwa Hospitalini hapo waliweza kumuanzishia Matibabu kwa
haraka na kwamba sasa hali yake inaendelea vizuri.
BAGAMOYO
KWANZA BLOG ilimtafuta Afisa Mali asili wa Wilaya ya Lindi, Victor Shau, ili
kuzungumzia tukio hilo ambae amewaomba wananchi wanaoishi maeneo
yanayokaribiana na Msitu wa Tarafa ya Rondo, kuchukuwa tahadhari ikiwa ni
pamoja na kutotembea hovyo nyakati za usiku, kutoka Kijiji kimoja kwenda
kingine ili kulinda usalama wa maisha yao.
No comments:
Post a Comment