Saturday, May 11, 2019

MANISPAA YA LINDI KUANDAA MPANGO WA USAFIRI KWA WANAFUNZI.

 NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Manispaa ya Lindi Mkoani humo imesema inaanda mpango maalumu wa kuwasaidia Usafiri wanafunzi wanaoishi mbali na maeneo ya shule.


Hayo yamesemwa jana Mei 10, 2019 na mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga mbele ya Mkuu wa Mkoa huo alipokuwa ametembelea katika shule ya Sekondari ya Mingoyo iliyopo kata ya Mnazi mmoja manispaa ya Lindi.


Ndemanga alisema kama Halmashauri imeamua kuandaa mpango huo kwa kuwa wamebaini kuwepo kwa wanafuzi ambao hutembea umbali mrefu kutoka maeneo wanayoishi na kuja shuleni.


Ndemanga alisema wapo baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika baadhi ya Shule za Sekondari katika Manispaa hiyo ambao hutembea umbali wa zaidi ya kilomita 16 wakati wa kwenda na kurudi shuleni.


Elody Osward (14) ni miongoni mwa wanafunzi wanaosoma katika shule ya Mingoyo iliyopo halmashauri ya Manispaa ya Lindi anaishi katika mtaa wa mayani ambae hulazimika kutembea umbali wa kilomita 16 wakati wa kwenda na kurudi shuleni.


Osward alisema kuwa Changamoto anayokabiliana nayo wakati anakwenda shuleni ni kukutana na wanyama wakati akiwa njiani ambao analazimika kuwafukuza ama kujificha ili kuwaacha wapite wanyama hao ndipo yeye aendelee na safari yake ya kwenda shuleni ama kurudi nyumbani.


Hata hivyo Osward alisema kitendo hicho cha yeye kutembea umbali mrefu kunamfanya ajihisi kuchoka anapokuwa darasani ambapo aliiomba serikali kumsaidia chombo cha usafiri ambacho kitaweza kumuwezesha kufika kwa wakati shuleni hapo.


Nae mkuu wa Shule ya Sekondari Mingoyo, Mwichande Lihoma, alimuelezea Osward kuwa ni mwanafunzi hodari na anaeonakana kupenda masomo kwani pamoja na kwamba anaishi mbali na Shule hiyo lakini hajawahi kukosa kufika shuleni na kwamba anapofika kwa kuchelewa huwa anafidia muda wake kwa kuchelewa kutoka Shuleni.


Alisema kitendo hicho cha kuchelewa kuondoka ni hatari kwake kwani hufika usiku sana nyumbani kwao.


Nae mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Jomary Satura, alisema kuwa katika kutekeleza mpango huo tayari wameshaagiza gari ndongo aina ya hice ambayo itakuwa inatumika kwa wanafunzi hao ambao wanaishi mbali na maeneo ya Shule.


Alisema gari hizo zitakapoanza kufanya kazi , zitaanzia katika Stendi kuu ya Mabasi ya Halmashauri hiyo na majira ya saa 12 Asubuh kuelekea Mto Mkavu na nyingine kuelekea Mkwaya

No comments:

Post a Comment