Monday, May 13, 2019

UWT PWANI WAANDAA KONGAMANO LA KUMPONGEZA RAIS DK. MAGUFULI KWA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM 2015 -2019

Mbunge wa viti maalumu wa kuteuliwa, Mama Salma Kikwete akizungumza katika kikao cha maandalizi ya kongamano la kumpongeza Rais Dk.John Magufuli na serikali kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2015 – 2018, kushoto ni mwenyekiti wa UWT mkoani Pwani,Farida Mgomi.( Picha na Mwamvua Mwinyi)
............................


NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA.

UMOJA wa wanawake Tanzania (UWT), mkoa wa Pwani umefanya mkutano maalumu wa maandalizi ya kongamano la kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kufuatia utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM 2015 – 2019 katika mkoa huo, ambapo unatarajiwa kufanyika hivi karibuni.


Mwenyekiti wa Uwt Mkoa wa Pwani, Farida Mgomi, akielezea juu ya kongamano hilo alisema, wamekutana wajumbe wa kamati maalumu kwa ajili ya kuzungumza namna bora jinsi ya kujipanga katika maandalizi hayo.


Aidha alisema, Rais Dk. Magufuli ni jemedari na kiongozi asiyeyumbishwa na mtu katika kulijenga Taifa kuelekea kwenye uchumi wa kati, amefanya mengi katika mkoa huo hasa  miradi mikubwa ya ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR), utengenezaji wa barabara za lami, ujenzi wa bwawa la umeme eneo la Rufiji, ujenzi wa viwanda na mradi mkubwa wa umeme.


“Sisi uongozi wa umoja wa wanawake wa Tanzania (UWT) wa chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani  tumepata wasaa wa kufanya mazungumzo na kupata namna nzuri ya kuandaa kongamano letu, ukiachia kumpongeza Rais Magufuli lakini pia kuwakutanisha wanawake wa mkoa huu na kupeana mbinu mbalimbali za kiuchumi”


“Lakini kupitia kongamano hilo pia wabunge wa viti maalum wa mkoa akiwemo Subira Mgalu, Hawa Mchafu na Zaynab Vullu watapata fursa ya kutoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kuanzia 2015 hadi 2019 kwa mkoa wetu wa Pwani”alielezea.


Hata hivyo Farida alifafanua kwa kusema kuwa, kinamama pia watapata elimu juu ya namna ya kutumia fursa za viwanda na mradi mkubwa wa Stigler's Gorge , katika kujikwamua kiuchumi .


Mbunge wa viti maalum wa kuteuliwa mama Salma Kikwete alikuwa miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Pwani ambae aliupongeza uongozi wa jumuiya hiyo kwa kuamua kufanya kikao kwa ajili ya maandalizi ya kongamano kubwa la kumpongeza Rais.


Aliahidi na kuwahakikishia jumuiya hiyo kuwa pamoja nao katika kuhakikisha kongamano hilo linafanyika na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

No comments:

Post a Comment