Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dkt John Pombe
Magufuli akipiga ngoma za bendi ya jeshi ya Mwenge Jazzz wana Paselepa wakati
wa kufunga Zoezi la medani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa
Pwani leo Septemba 30, 2016
...........................................
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Septemba, 2016
amefunga maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa
kushuhudia zoezi la medani liitwalo ''Amphibious Landing'' lililofanyika katika
Kijiji cha Baatini Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.
Zoezi hilo lililochukua muda wa wiki mbili,
limeshirikisha kamandi zote tano za JWTZ ambazo ni Nyika, Majini, Anga,
Kamandi ya Makao Makuu na Jeshi la Kujenga taifa limefanyika katika
ufukwe wa bahari ya Hindi na limetekelezwa kwa mfano wa mapambano ya kivita
yaliyohusisha kutua nchi kavu kutoka majini na kukomboa eneo lililotekwa.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo
Rais na Amiri jeshi Mkuu Dkt.John Pombe Magufuli amempongeza Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange pamoja na Makamanda na Wapiganaji wote wa
JWTZ walioshiriki katika zoezi hilo ambalo limefanywa kwa umakini, uhakika na
weledi wa hali ya juu.
''Kwa kweli nimefurahi na nimeamini tuna
wapiganaji wa kutosha katika maeneo yote, hii mikakati na mipango iliyotumika
inaonesha tuna jeshi imara na linaloaminika'' amesema Dkt. Magufuli.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu amewahakikishia
Makamanda na Wapiganaji wote wa JWTZ kuwa Serikali yake itahakikisha
inaendeleza na kuongeza zaidi juhudi zilizofanywa na Marais waliopita kwa
kuimarisha na kuwa na jeshi la kisasa linalotumia vifaa na teknoljia ya kisasa
na pia itahakikisha maslai ya askari yanaboreshwa.
Aidha, Dkt. Magufuli ametaka Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT) kuimarishwa zaidi na kujielekeza katika uzalishaji mali ikiwemo
uwekezaji katika viwanda.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye
pamoja na kuipongeza JWTZ amesema miaka 52 tangu kuanzishwa kwa Jeshi
hilo Watanzania wanashuhudia jeshi lao likiwa imara na makini zaidi kwa ajili
ya kulinda nchi.
Nae Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis
Mwamunyange amemshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli kwa
jitihada zake na nia yake ya kuliimarisha Jeshi na kuboresha maslai ya
Makamanda na Wapiganaji na ameongeza kuwa anajivunia kuwa kiongozi wa
Jeshi hilo.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi
wengine wakiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein
Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Katibu Mkuu Kiongozi wa
Zanzibar Abdulhamid Yahaya Mzee.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe
Magufuli, amemuagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange
kuwapa ajira za JWTZ askari mgambo wote walioshiriki zoezi la Amphibious
Landing.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Septemba, 2016
Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe
Magufuli, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na meza kuu wakipiga saluti
wakati wa wimbo wa Taifa wakati wa kufunga Zoezi la medani katika kilele cha
maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko
Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016.
Ndege vita zikipita angani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa
Pwani leo Septemba 30, 2016.
Vifaru vinavyopita baharini na nchi kavu vikiwa katika zoezi la
"Ambhibious Landing" katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52
ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa
wa Pwani leo Septemba 30, 2016.
Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Zanzibar
Dkt. Ali Mohamed Shein na meza kuu wakipiga makofi wakati wa Zoezi la medani
katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016. PICHA
ZOTE NA IKULU.