India imeipatia Tanzania dola za
Kimarekani milioni 500 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili kukuza ushirikiano
wa kiuchumi baina nchi hizi mbili.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
katika dhifa ya kitaifa aliyomwandalia mgeni wake, Waziri Mkuu wa India,
Mheshimiwa Narendra Modi.
“Tunaishukuru
India ambayo imeonyesha utayari wa kushirikiana nasi kiuchumi katika kilimo,
TEHAMA, maji, Elimu, Afya na Ulinzi,” amesema Rais Magufuli.Rais Magufuli pia
amesema ushirikiano wetu na India utatoa fursa kwa Tanzania kutimiza azma yake ya
kuwa na uchumi wa viwanda kwani katika ziara hii Waziri Mkuu ameambatana na
wafanyabiashara takriban 50 ambao wanaangalia fursa za kibiashara hapa nchini.
“India ni mdau wetu mkubwa wa
kibiashara na uhusiano huu umekuwa ukikua kwani mauzo ya bidhaa za
Tanzania nchini India yameongezaka toka thamani ya dola za kimarekani
milioni 187 mwaka 2005 hadi dola bilioni 1.29 mwaka 2015,”alisema Rais
Magufuli.Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa India itatoa fedha kwa nchi ya
Tanzania kwa ajili ya kilimo cha Dengu ambayo ni fursa ya ajira kwa watanzania
na kuinua kipato cha wananchi.
Rais Magufuli ameeleza kufurahishwa
kwake na miradi ya India ikiwemo mradi unaojulikana kama Making India, mradi
ambao unatumia malighafi zinazopatikana nchini na kutumia nguvu kazi ya nchini
ambao utapunguza tatizo la ajira katika Taifa la Tanzania.
Amebainisha kuwa India iko tayari
kushirikiana na Tanzania kwenye miradi ya gesi ikizingatiwa kuwa aina mbali
mbali za gesi zinazidi kugunduliwa hapa nchini. Katika suala la gesi India iko
tayari kutoa utaalamu na wataalamu kwa ajili miradi ya gesi.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa India ,
Mhe. Narendra Modi ameishukuru Tanzania kwa ukarimu alioupata hapa nchini na
akaahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili.Amesema
India italeta watu wake, utaalaamu na teknolojia yake kwa Tanzania, jambo
ambalo litaongeza ushirikiano wa kiuchuni kati India na Tanzania.
Waziri Mkuu huyo amemaliza ziara yake
ya kiserikali ya siku mbili nchini na kuondoka kuendelea na ziara katika
nchi nyingine za Ukanda wa Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment