MGOMBEA NAFASI YA MWENYEKITI WA
CCM
1.0. MAISHA YAKE
Ndugu John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa
Oktoba 29, mwaka 1959 katika kijiji cha Chato, Wilayani Biharamulo katika Mkoa
wa Kagera. Hivi sasa Chato ni Wilaya katika Mkoa wa Geita. Ndugu Magufuli ni
Daktari wa Falsafa (PhD) ya Kemia. Ana mke na watoto saba.
Alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba,
2015 kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (C.C.M). Aliapishwa na kuanza rasmi
majukumu yake ya kuiongoza Tanzania tarehe 5 Novemba, 2015.
Tangu ameingia madarakani, Rais Dkt.
Magufuli, ameonesha kuwa ana sifa zote muhimu za uongozi. Ana dira, maono na
malengo kuhusu anakotaka Taifa liende. Ana mikakati ya kutekeleza dira na maono
yake. Haogopi kufanya maamuzi makini. Ana kiu ya kuona Taifa linapata
maendeleo. Amejipambanua kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge na dhamira yake kubwa
ni kuona wananchi wanapata huduma bora za jamii na kero zao zinaondoka.
2.0. ELIMU NA MAFUNZO
Rais Dkt. Magufuli alianza elimu ya msingi
katika Shule ya msingi Chato mwaka 1967 na kumaliza mwaka 1974. Mwaka 1975
alianza masomo ya sekondari katika Shule ya Seminari ya Katoke Mkoani Kagera.
Mwaka 1977 alihamia shule ya sekondari ya Lake iliyopo Mkoani Mwanza
na kuhitimu kidato cha Nne mwaka 1978. Kuanzia mwaka 1979 hadi 1981
alifanya masomo ya kidato cha Tano na Sita katika shule ya Sekondari ya
Mkwawa Mkoa wa Iringa .
Mwaka 1981 hadi 1982 alisoma Chuo cha
Ualimu Mkwawa na kuhitimu Stashahada ya Ualimu ya Masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwezi Julai hadi Disemba mwaka 1983, Dkt. Magufuli alipata mafunzo ya
kijeshi katika Jeshi la kujenga Taifa kikosi cha Makutupora mkoa wa
Dodoma. Mwezi Januari hadi Machi 1984 alihamishiwa kikosi cha mafunzo Jeshi la
Kujenga Taifa Makuyuni, Arusha. Mwezi huo wa Machi alihamia kikosi cha
Jeshi la Kujenga Taifa Mpwapwa Dodoma na kumaliza mafunzo mwezi Juni 1984.
Mwaka 1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar
es salaam kusoma Shahada ya kwanza ya Sayansi na Ualimu akijikita katika masomo
ya Kemia na Hisabati. Alitunukiwa Shahada hiyo mwaka 1988. Mwaka 1991
hadi 1994 alisoma na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika fani ya Kemia
iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Chuo Kikuu cha Salford cha
Uingereza. Mwaka 2006 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili
ya Shahada ya Uzamivu katika Fani ya Kemia na kufanikiwa kuhitimu mwaka 2009.
3.0. UZOEFU WA NDANI YA
SERIKALI
Baada ya kuhitimu masomo yake ya Stashahada
ya Ualimu, mwaka 1982 hadi 1983 Dkt. Magufuli alikuwa Mwalimu katika shule ya
Sekondari ya Sengerema iliyopo Mkoani Mwanza akifundisha masomo ya Kemia na
Hisabati. Mwaka 1989 alijiunga na Chama Cha Ushirika cha Nyanza Mkoani
Mwanza, ambapo alifanya kazi kama Mkemia Mkuu hadi mwaka 1995.
Mwaka 1995 alichaguliwa kuwa Mbunge wa
Jimbo la Biharamulo Mashariki Mkoa wa Kagera. Baada ya Uchaguzi, Rais wa
Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa
Wizara ya Ujenzi nafasi ambayo aliitumikia hadi mwaka 2000. Mwaka
2000 alichaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki
lakini mara hii akipita bila kupingwa. Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa
Waziri kamili wa Wizara ya Ujenzi hadi mwaka 2005.
Mwaka 2005 Rais Dkt. Magufuli alichaguliwa
kwa mara ya tatu kuwa mbunge wa jimbo la Biharamulo Mashariki, kwa mara
nyingine akipita bila kupingwa. Baada ya uchaguzi, Rais wa Awamu ya Nne,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008 ambapo alihamishiwa
Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi hadi hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa
mara ya nne kuwa Mbunge lakini, kufuatia mgawanyo wa majimbo
uliofanyika, mara hii katika Jimbo jipya la Chato. Baada ya uchaguzi,
aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.
Wakati akiwa Mbunge na Waziri, Dkt.
Magufuli amefanya shughuli na kushika nyadhifa kadhaa ndani na nje ya nchi.
Mwaka 2014, Dkt. Magufuli alishiriki katika Bunge Maalum la Kutunga Katiba Mpya
akiwa ni Mjumbe wa Bunge hilo. Aidha, wakati akiwa Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliweza kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza
(Co-Chair) wa Mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi
(UN-Habitat).
Tarehe 25 Oktoba, 2015 Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
tarehe 5 Novemba, 2015 aliapishwa kushika rasmi wadhifa huo.
4.0. UZOEFU WA UONGOZI NDANI YA CHAMA
Rais Dkt. Magufuli alijiunga na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) mwaka 1977. Amekuwa Mwanachama mwaminifu na ameshika nafasi
mbalimbali za uongozi ndani ya Chama. Nafasi alizowahi kushika ni pamoja na
kuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
Wilaya, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa,
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.
Sambamba na kushika nafasi mbalimbali za
uongozi, Dkt. Magufuli mara zote alijitoa kukitetea Chama na kuhakikisha
kinapata ushindi. Alishiriki kikamilifu kuwafanyia kampeni wagombea wa CCM
katika Chaguzi Ndogo zilizofayika katika majimbo ya Busanda, Biharamulo
Magharibi na Igunga na kupata ushindi. Katika Mkutano Mkuu wa CCM wa
tarehe 11 – 12 Novemba mwaka 2012, Dkt. Magufuli alikuwa miongoni mwa Mawaziri
wachache waliopata fursa ya kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya Chama ya Mwaka 2010 – 2015. Alielezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani,
hususan katika sekta ya miundombinu.
Tarehe 11 mwezi Julai, 2015 Mkutano Mkuu wa
Taifa wa CCM ulimchagua na kumteua Dkt. Magufuli kuwa mgombea Urais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Aliinadi vyema Ilani ya uchaguzi ya CCM (2015)
na kukiwezesha Chama kupata ushindi mkubwa. Tarehe 25 Oktoba, 2015 alichaguliwa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nafasi hiyo imemwezesha
kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa.
5.0. UFANISI KATIKA UONGOZI
Dkt. Magufuli ni kiongozi mnyenyekevu,
aliye na hofu ya Mungu, mkweli, mtekelezaji wa ahadi, mwadilifu, shupavu,
mahiri, mbunifu, mtafiti, mchapakazi na mtetezi wa wanyonge. Ni kiongozi mpenda
haki na mchukia dhuluma, rushwa, ufisadi na ubaguzi wa aina yoyote ile.
Ni kiongozi mwenye msimamo na mtetezi wa yale anayoyaamini.
Katika nyadhifa zote alizopata kutumikia
alifanya kazi kwa uadilifu na umahiri mkubwa. Amejidhihirisha na kujipambanua
kuwa ni mfuatiliaji na msimamizi wa sheria. Akiwa Mwalimu Sengerema Sekondari
aliwezesha wanafunzi wote wa darasa lake kufaulu masomo ya Hesabu na Kemia
aliyokuwa akiyafundisha. Akiwa Mkemia Mkuu wa Chama cha Ushirika cha Nyanza
alisimamia vyema ubora wa uzalishaji wa mafuta ya Pamba na kuifanya Kampuni ya
Nyanza kuwa mzalishaji mzuri wa mafuta ya Pamba.
Akiwa Waziri wa Ujenzi anakumbukwa kwa
kubuni na kusanifu miradi ya ujenzi wa barabara, kusimamia vizuri matumizi ya
fedha na kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango na kwa wakati
uliopangwa. Uwezo wake katika kubuni na kusanifu miradi ya barabara uliigwa na
nchi majirani, ikiwemo Kenya. Ameondoka Wizara ya Ujenzi akiwa amesimamia
ujenzi wa zaidi ya Kilometa 17,000 za barabara za lami, madaraja makubwa zaidi
ya 14 na madaraja madogo madogo zaidi ya 7,000 na vivuko. Aidha, alisimamia
vizuri taasisi mbalimbali za Makandarasi, Wahandisi, Wabunifu na Wakadiriaji
Majengo.
Dkt. Magufuli pia anasifika kwa uwezo wake
mkubwa wa kuweka kumbukumbu ya kazi zake. Akiwa Wizara ya Ujenzi aliweza
kutaja majina ya barabara zilizojengwa au zilizokuwa katika hatua za ujenzi,
urefu wake, majina ya wakandarasi pamoja na gharama za ujenzi bila kusoma
mahali popote. Wakati wa Rais Mstaafu Benjamini William Mkapa alimwita
“Askari wa Mwavuli”.
Akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi alisimamia upimaji wa ardhi za vijiji na viwanja vya makazi, na
kushughulikia migogoro mingi ya ardhi iliyowahusu wananchi wa maisha ya chini.
Wakati akiwa Waziri wa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi alikuwa
maarufu wa kutambua na kutaja idadi ya mifugo, kama vile samaki,
ngómbe, mbuzi, kondoo, kuku, mbwa n.k. Kitendo cha kukamata meli ya
kichina iliyokuwa ikivua samaki kwa wizi ndani ya Bahari Kuu ya Hindi eneo la
Tanzania kilidhihirisha uzalendo kwa Taifa lake. Rais Mstaafu wa Awamu ya
Nne Dkt. Kikwete alimpachika jina maarufu la “Tingatinga”.
Sifa hizi nzuri ameendelea nazo hata baada
ya kuchaguliwa kuwa Rais. Katika miezi michache ya uongozi wake amethibitisha
anatekeleza ahadi. Aliahidi kutoa elimu bila malipo na kuanzisha Mahakama ya
Mafisadi. Ameweza kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma kwa kuondoa
watumishi hewa na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa umma wasio waaminifu,
wala rushwa, wazembe na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Ameweza
kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya
Serikali. Kwa hakika Dkt. Magufuli anaakisi uongozi bora unaopaswa kuigwa na
viongozi wengi Barani Afrika na Dunia.
6.0. DHIMA YA UONGOZI WA SERIKALI YA AWAMU
YA TANO 2015 – 2020) NA MALENGO YAKE MAHSUSI
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka
2015 – 2020 inazielekeza serikali zake kutumia nguvu zake zote kuendelea
kupambana na changamoto kubwa nne;- Kwanza kuondoa umaskini, Pili, kupunguza
tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, Tatu, kuendeleza vita dhidi ya adui
rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, na Nne, kuendelea kudumisha amani, ulinzi
na usalama wa maisha ya Watanzania na mali zao.
Sambamba na kutekeleza mambo hayo makubwa
manne, kipindi cha Kampeni na wakati akizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015 Rais Dkt. Magufuli alitaja malengo
mahsusi ya Serikali ya Awamu ya Tano. Malengo hayo ni haya yafuatayo:
· Kudumisha Muungano, Amani na
Umoja wa Tanzania. Serikali haitamwonea aibu mtu mwenye nia ya kuvunja Muungano
na kuvuruga amani na mshikamano katika nchi. Hili alilidhihirisha vizuri wakati
wa uchaguzi wa marudio huko Zanzibar, kwani Uchaguzi ulifanyika kwa amani na
utulivu.
· Kujenga Uchumi wa Viwanda
ili kufikia azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kulingana na malengo ya
Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Viwanda vinalengwa ni vyenye kutumia
nguvu kazi kubwa, malighafi za ndani ya nchi, kuzalisha bidhaa kwa ajili ya
soko la ndani na nje ya nchi. Nia ni kukabiliana na tatizo la ajira na
umasikini;
· Kuongeza kasi ya ujenzi wa
miundombinu ya kiuchumi, hususan miundombinu ya usafiri na nishati;
· Kuimarisha huduma za jamii,
hususan elimu, Afya na Maji. Lengo ni kuhakikisha huduma hizo zinapatakana sio
tu kwa urahisi bali pia kwa ubora unaostahili ili kukabiliana na maadui ujinga,
umaskini na maradhi;
· Kusimamia uwajibikaji wa
utumishi wa umma na kuondoa urasimu ndani ya Serikali. Lengo ni kuhakikisha
watumishi wa umma wanafanya kazi kwa ueledi, uadilifu na kujituma ili
kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati;
· Kuimarisha usimamizi
wa rasilimali za nchi, ikiwemo kuhifadhi mazingira na kuzidisha vita dhidi ya
ujangili. Lengo ni kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha watu wote wa
kizazi cha sasa na kijacho. Aidha, ukusanyaji wa mapato ya Serikali na udhibiti
wa matumizi ya Serikali nao utaimarishwa;
· Kusimamia utawala
bora unaozingatia sheria na haki za binadamu. Jitihada za makusudi zitaelekezwa
katika kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, dhuluma na uonevu wa aina
yoyote. Aidha, maslahi ya makundi mbalimbali katika jamii, ikiwemo wanawake,
wazee, watu wenye ulemavu na watoto yatalindwa. Kwa upande mwingine, wananchi
watahimizwa kuheshimu na kufuata sheria za nchi;
· Kulinda usalama wa
raia na mali zao kwa kupambana na uhalifu, ikiwemo wizi, ujambazi, tatizo la
dawa za kulevya n.k.
· Kudumisha na
kuendeleza ujirani mwema, mahusiano mema na Mataifa mengine duniani pamoja na
Mashirika ya Kimataifa na Kikanda;
· Kuendeleza na
kusimamia vizuri shughuli za michezo, sanaa, burudani na utamaduni, ikiwemo
kukuza lugha ya Kiswahili.
HITIMISHO
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo ya
kiuchumi na kuwataka watanzania washiriki kufanya kazi kwa bidii na
maarifa ndani ya falsafa ya HAPA KAZI TU. Dhamira hii inakusudia
kuwezesha Taifa letu kufikia Uchumi wa Kati uaoongozwa na Viwanda ili kutimiza
malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment