Tuesday, July 12, 2016

RAIS, DKT. JOHN MAGUFULI AWATAKA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI, WAKAONDOE KERO ZA WANANCHI.


 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni na kuwataka kuwatumikia wananchi ikiwemo kuondoa kero zinazowakili wananchi katika maeneo yao ikiwemo utitiri wa kodi hasa kwenye bidhaa wanazozalisha.Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angella Kairuku na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan. wakati wa hafla ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam. 




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya hapa nchini kufanya kazi za kuwaletea maendeleo wananchi na kuondoa kero zinazowakabili kwa kujiamini, uadilifu na uaminifu.

Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo tarehe 12 Julai, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam muda mfupi kabla ya wakurugenzi hao wa halmashauri kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo limeendeshwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mhe. Rais Magufuli amesema katika kutekeleza jukumu hilo la kuwaletea wananchi maendeleo na kuondoa kero zinazowakabili, wakurugenzi hao hawana budi kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo ahadi ambazo serikali ya awamu ya tano imezitoa, wakiongozwa na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 - 2020.

Aidha, amesema wakurugenzi wote wa halmashauri wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na amewataka kutosita kuchukua hatua dhidi ya watendaji ambao wamejigeuza kuwa miungu watu na wanawanyanyasa wananchi.

"Wapo watendaji wa kata ambao ni miungu watu, wanachonganisha wananchi na serikali, katumieni madaraka mliyonayo kuwaondoa kazini" Amesema Rais Magufuli

Mhe. Rais Magufuli pia amewataka wakurugenzi hao kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya serikali na ametumia nafasi hiyo kuagiza wizara zote kuanza kutumia mashine za kielektroniki (EFD) katika ukusanyaji wa mapato kwenye taasisi zote ambazo zinakusanya maduhuli.

Dkt. Magufuli amewasisitiza wakurugenzi hao kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utoaji wa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, ambapo kila mwezi serikali hutoa shilingi bilioni 18.777 na ametaka tabia ya wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na wafanyabiashara ama wanasiasa kujinufaisha kupitia zabuni za serikali ikome.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambao walikuwepo wamewataka wakurugenzi hao wa halmashauri kuwa watumishi bora, kusimamia vizuri rasilimali za halmashauri na kushirikiana na viongozi wa mkoa na wilaya katika halmashauri zao.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
12 Julai, 2016

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan akiongea na wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya (Hawapo pichani) walioteuliwa hivi karibuni na kusisitiza kwenye matumizi ya Kanuni, Sheria na Taratibu katika kutimiza majukumu yao. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angella Kairuku. wakati wa hafla ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni.

 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Majaliwa Kassim akiongea na Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa dhumuni la kuwaletea wananchi maendeleo.Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angella Kairuku, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa hafla ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma kwa wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angella Kairuku akiongea na wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni.

 

Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni wakila kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma. Wakati wa hafla ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni, iliyofanyika Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment