Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Maudhui, Joseph Method Mapunda. |
Kamati ya maudhui ya Mamlaka ya mawasiliano
nchini TCRA, imekionya kituo cha utangazaji cha Clouds Television kufuatia
kuzungumzia ushoga katika kipindi chake cha TAKE ONE, kilichorushwa tarehe
28/06/2016 ambapo mwendeshaji wa kipindi hicho alimualika mtu aliyejitambulisha kwamba yeye ni shoga.
Akisoma maelezo ya hukumu yaliyochukua dakika 27,
katika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Makamu Mwenyekiti wa
kamati ya maudhui ya TCRA, Joseph Method Mapunda alisema kituo hicho cha
Television kilikiuka kanuni na maadili ya utangazaji kutokana na mambo yafuatayo
1. Kipindi
kimeonyesha waziwazi jinsi ushoga unavyofanyika pamoja na mbinu zinazotumika.
2. Shoga
aliyehojiwa hajuti kujiingiza katika katika tabia hii mbaya hasa pale anaposema
kuwa, ataendelea kufanya ushoga hadi mwisho wa maisha yake.
3. Lugha
iliyotumika katika mahojiano haina staha.
4. Tabia
ya ushoga inaanzia shuleni.
5. Mtangazaji alikuwa anauliza maswali
yanayoashiria kushabikia ushoga.
Aidha, Mapunda aliongeza kuwa, kamati hiyo ya
maudhui ya TCRA ilibaini kuwa, kipindi kilikuwa hakina ubora kwakuwa maswali
mengi aliyokuwa anauliza mtangazaji yalilenga kuhamasisha ushoga ikiwa ni
pamoja na matumizi ya lugha isiyo na staha.
Aliongeza kuwa, kila mwenye leseni ya utoaji
huduma za utangazaji lazima ahakikishe kuwa, vipindi vyake vinaepuka kufuru
katika jamii na vizingatie unyeti wa imani za kidini na utamaduni katika jamii.
Alisema watanzania kwa kuzingatia imani zao za
kidini na utamaduni hawakubaliani na ushoga.
Katika utetezi wake Clouds Television walisema
kuwa jamii imebadilika kwa kiasi kikubwa na kwamba ukubwa tatizo la ushoga lipo
kwenye mitandao ya kijamii hadi kufikia matangazo kutolewa katika mitandao
hiyo.
Aidha, Clouds Television walikiri kuwa, ushoga ni
kitu kibaya na kuongeza kuwa ifike wakati mtu akifanya kitendo cha ushoga
aogopwe.
Makamu mwenyekiti huyo wa kamati ya maudhui ya
TCRA alisema kuwa baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi
yaliyotlewa na uongozi wa Clouds Television, kamati ya maudhui imeridhika kuwa
mada ya ushoga kupitia kipindi cha TAKE ONE kilichorushwa hewani tarehe
28/06/2016 kilikiuka baadhi ya kanuni za huduma za utangazaji (Maudhui) 2005,
ambazo ni 5(b), 5(c), 5(d), 15(c) na 16(2).
Mapunda aliongeza kuwa hukumu iliyotolewa kwa
Clouds Television ni kuwa
1. inatakiwa
kuwaomba radhi watazamaji wake na watanzania kwa ujumla kutokana na kuwakwaza
pamoja na kuwasababishia usumbufu kwa kurusha mada inayoongelea ushoga kwa
namna upotoshaji kupitia kupitia kipindi cha TAKE ONE kilichorushwa tarehe
28/06/2016.
Aidha, Taarifa ya
kuomba radhi itoke siku tano mfululizo kwenye Taarifa za habari za saa 1:30
usiku na saa 5:00 usiku kuanzia siku ya kusomwa hukumu na uthibitisho wa
taarifa hizo uwasilishwe Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania siku ya jumatano ya
tarehe 13/07/2016 kabla ya saa 10:00 jioni.
2. Clouds
Television inatakiwa kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza na kuhakikisha
inazingatia kanuni zote za utangazaji nchini katika kutekeleza majukumu yake ya
utangazaji.
3. Kamati
ya Maudhui, inawaonya vikali Clouds Television kwa kukiuka kanuni za utangazaji
(Maudhui), 2005 na 5(b), 5(c), 5(d), 15(c), na 16(2).
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Clouds Television Ruge Mutahaba alisema wamepokea kwa masikitiko
hukumu hiyo kwakuwa lengo la kipindi hicho ni kuielimsha jamii madhara ya
ushoga na si vinginevyo.
No comments:
Post a Comment