MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Jerry
Muro (pichani) amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja na
kutozwa faini ya Sh. Milioni 3, baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), kilichokaa leo kwenye Makao Makuu ya Shirikisho hilo,
chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde
Muro amefungiwa baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka mawili
kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF mbele ya Kamati ya hiyo, ambayo ni
kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa
faini ya Sh. Milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi
leo, akahukumiwa kutengana na kutojihusisha na masuala ya soka kwa mwaka mmoja,
wakati shitaka lingine ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo
wa Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.
Katika shitaka hilo, Jerry alidaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga
kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao na kutowapa nafasi watani wao wa
jadi (Simba) kuingia kwenye mchezo huo ambao timu yake ilifungwa bao 1-0 na
Mazembe Juni 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Jerry Muro alifanikiwa kuishinda TFF katika shitaka la
kupingana na maamuzi ya shirikisho hilo juu ya masuala ya utoaji wa haki za
matangazo ya Televisheni.
“Kamati ilisikiliza kwa makini taarifa zake alipokuwa anazungumza
na vituo vya Redio na kugundua alikuwa sahihi, hivyo hapa hana hatia,”kimesema
chanzo.Hata hivyo, Jerry Muro amehukumiwa wakati mwenyewe hakuwepo kwenye kikao
na inadaiwa hakutoa taarifa ya maandishi juu ya kutohudhuria kwake.
Badala yake, imeelezwa Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit alifika
mapema leo kabla ya kikao kwa ajili ya kutoa taarifa ya mdomo kwamba Muro
amekwenda kwao Kilimanjaro kusafisha makaburi ya wazee wake.
Lakini Kamati ikaamua kuendelea na kikao kwa mujibu wa kanuni na
hatimaye kuchukua hatua ilizochukua. Hata hivyo, Muro ana haki ya kukata rufaa
Kamati ya Rufaa ya TFF.
No comments:
Post a Comment