Thursday, July 7, 2016

WANANCHI BAGAMOYO, WAMPONGEZA MKUU WA WILAYA KWA KUSIMAMIA AMANI NA UTULIVU KIPINDI CHA SIKUKUU.



Wananchi wa Bagamoyo wamempongeza mkuu wa wilaya ya hiyo, Alhaji, Majid Hemed Mwanga kwa mikakati mizuri iliyosaidia kuondoa vurugu katika sikukuu ya Eid el fitri ya mwaka huu.

Wakizungumza na bagamoyokwanza blog, kwa nyakati tofauti mjini Bagamoyo, wananchi hao walisema kuwa ni jambo la kupongeza kwa ulinzi na usalama namna ulivyoimarishwa katika mji wa Bagamoyo hasa katika kipindi hiki cha sikukuu ya Eid elfitri.

Walisema mwaka huu sikukuu imekuwa nzuri kwakuwa mji wa Bagamoyo umekuwa tulivu huku wananchi wakitembea bila ya bugudha yoyote ukilinganisha na miaka iliyopita ambapo kumekuwa na tabia ya makundi kutoka nje ya Bagamoyo ambao hufika Bagamoyo na kufanya fujo za aina mbalimbali ikiwemo kupora watu, kuwadhuru na kuharibu mali za watu



Miraji Nambole, mkazi wa Bagamoyo alisema Hali hiyo imetokana na juhudi za mkuu wa  wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga ambae ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya, ambapo alitangaza kuwa  atakaefanya fujo atachukuliwa hatua za kisheria.
 

Nae Hamadi Athumani, alisema kuwa kila kitu kinawezekana endepo kitawekewa mikakati na mipango thabiti ya utekelezaji na kuongeza kuwa, katika hili serikali ya wilaya imejipanga na  imefanikiwa ambapo wananchi wameweza kufarahia sikukuu bila ya vurugu yoyote.




Kwa upande wake Diwani wa kata ya Dunda Dicksoni Makamba, alisema kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano uliopo kati ya mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, ambae ni mkuu wa wilaya na vikosi vya ulinzi na usalama vilivyopo katika wilaya hiyo.

Aliseme utekelezaji wa majukumu yoyote unahitaji ushirikiano na kwamba hata mafanikio hayo ya kuzuia fujo katika mji wa Bagamoyo yamepatikana kutokana na ushirikiano.

Hata hivyo aliwashukuru wananchi wa Bagamoyo kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha amani na utulivu vinachukua nafasi yake.

Kata ya Dunda ndiyo inayopokea wageni wengi siku za siku za sikukuu kwakuwa kata hiyo ipo katika ufukwe wa Bahari ya Hindi ambayo watu wengi hupenda kutembelea.

Siku moja kabla ya sikukuu ya Eid elfitri, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Hemed Mwanga alitoa onyo kwa yeyote atakaesababisha fujo katika kipindi cha sikukuu huku magari ya abiria yanayoingia Bagamoyo kutakiwa kuwa na vibali vya kuingia Bagamoyo hali iliyosaidia kuondoa msongamano wa makundi yenye kuleta fujo siku za sikukuu katika mji wa Bagamoyo.



1 comment:

  1. Hongereni sana wana Bagamoyo kwa kuendeleza mshikamno na utulivu. Amani idumu.Hongera pia Mwanahabari Shomari kwa kutuhabarisha.

    ReplyDelete