Monday, July 11, 2016

BILIONI 1.3 ZAKUSANYWA DARAJA LA KIGAMBONI NDANI YA MIEZI 2.


 


Jumla ya shilingi bilioni 1.3 zimekusanywa kutoka Daraja la Nyerere lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam kupitia tozo mbalimbali zinazolipwa na vyombo vya usafiri vinavyopita darajani hapo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Prof. Godius Kahyarara wakati akieleza mapato yaliyopatikana kwenye daraja hilo tangu lilipofunguliwa rasmi Mei 14 mwaka huu.

Prof. Kahyarara alisema kuwa fedha hizo zimekusanywa kupitia tozo za magari yakiwemo magari binafsi, magari ya abiria, magari ya mizigo, pikipiki na bajaji zinazopita darajani hapo kila siku. Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi wa Daraja la Nyerere, Bw. Gerald Sondo alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na uongozi wa daraja wana mpango wa kuboresha huduma za malipo ili watumiaji wa daraja hilo waweze kulipa tozo kwa kutumia kadi za kielektroniki.

“Hivi karibuni tunatarajia kuanzisha mfumo wa malipo kwa kutumia kadi za kielektroniki ambapo madereva wa vyombo vya usafiri watakuwa wanatumia kulipa tozo pindi wanapopita darajani” alisema Sondo.

Aliongeza kuwa mfumo huo utapunguza changamoto ya kupokea pesa taslimu mkononi kwa wanaokusanya mapato darajani hapo, hivyo kuondoa usumbufu wa chenji na kuimarisha usalama wa fedha hizo. Aidha, Bw. Sondo alieleza kuwa mfumo huo pia utawawezesha watumiaji wa daraja hilo kulipa tozo kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ya kufanya miamala ya fedha kupitia benki na mitandao mbalimbali ya simu.

Alisema kuwa kwa sasa idadi ya magari, pikipiki na bajaji zinazopita darajani hapo ni kati ya elfu 8 hadi elfu 10 kwa siku na wanalipa tozo kulingana na aina ya chombo cha usafiri. Kwa upande wa waenda kwa miguu na waendesha baiskeli hawalipi gharama yoyote wanapopita kwenye daraja hilo.

Akieleza kuhusu usalama wa daraja na watumiaji wake, Bw. Sondo alisema kuwa ulinzi ni wa uhakika kwa saa 24 kila siku kwani kuna askari wa kutosha pamoja na kamera zinazosaidia zoezi hilo. Pia alisema kuwa wanaandaa kanuni za matumizi ya daraja ikiwemo faini za uharibifu, uchafuzi wa mazingira, matumizi mabaya ya njia na lugha za matusi.

No comments:

Post a Comment