Serikali ya India na Tanzania zimesaini
mikataba ya miradi ya maendeleo katika sekta za maji, kilimo, viwanda,
teknolojia ya habari na mawasiliano na afya katika kuimarisha mahusiano ya nchi
hizo mbili ili kusaidia wananchi wake.
Mikataba hiyo imesainiwa leo, wakati
Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi alipokua akifanya mazungumzo na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar
es Salaam.
Mikataba wa kwanza uliosainiwa
inahusisha mradi wa kusambaza maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Aidha, mkataba wa pili unahusisha mradi
wa kusambaza maji Zanzibar ambao unatarajiwa kugharimu dola za kimarekani
milioni 92 ambapo mradi huo unatarajiwa kufikia miji 17 nchini na mkataba
mwingine utahusisha mafunzo ya ufundi yatakayosaidia kuzalisha wataalamu
mbalimbali.
“Lengo letu ni kusaidiana na
kuimarisha mahusianao yetu katika kukuza uchumi na kutengeneza fursa mpya za
ajira kwa wananchi wetu” alisema Waziri Modi.
Waziri Modi aliongeza kuwa Serikali ya
India itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali
ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa biashara na hatimaye kukuza
uchumi wa nchi hizo.
Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alisema Serikali India imekua na
ushirikiano mzuri na Tanzania hasa katika masuala ya maendeleo ambapo imeweza
kuwekeza nchini kiasi shilingi za Kimarekani dola bilioni 2.4 na kuzalisha
ajira 54,176.
Baadhi ya misaada iliyotolewa na
Serikali ya India ni pamoja na mashine ya vipimo vya ugonjwa wa kansa
katika hospitali ya Bugando, itakayosaidia wakazi wa kanda ya ziwa na nchi
nzima kwa ujumla pamoja na kuongeza na kuimarisha ushirikiano kati ya Shirika la
viwanda vidogo vigodo la India kushirikiana na Tanzania katika kukuza viwanda
vidogo na vya kati nchini.
Katika masuala ya teknolojia ya habari
na mawasiliano, Serikali hiyo imeahidi kuleta wataalamu wao nchini Tanzania kwa
lengo la kutengeneza program mbalimbali ili kuisaidia Tanzania katika masuala
ya ulinzi wa mitandao pamoja na kutengeneza namna bora za ukusanyaji wa mapato
ya nchi.
Katika masuala ya viwanda, Serikali ya
India imeahidi kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu
zitakazotibu magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria, figo na
kisukari, ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifaa tiba vitakavyotumika katika
hospitali mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza gharama ya kununua vifaa
hivyo nje ya nchi.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa nchi
ya India ina uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo hasa jamii ya kunde hivyo
akawataka wakulima kutumia fursa hiyo kuzalisha mazao hayo kwa wingi.
“India inauhitaji wa tani 200 za mazao
jamii ya kunde, wakulima mnatakiwa kuzalisha mazao hayo kwa wingi kwa vile
tayari kuna soko la uhakika, na tutahakikisha madalali hawatakuwepo ili mkulima
asikandamizwe” alisema Rais Magufuli.
Katika sekta ya uwekezaji nchini, India
ni nchi ya tatu kwa uwekezaji Tanzania ikifuatiwa na Uingereza pamoja na China.
No comments:
Post a Comment