Tuesday, January 29, 2019

WASAUDIA WATUA TANZANIA KUTAFUTA FURSA ZA KUWEKEZA KATIKA VIWANDA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wasaudia watafuta Fursa za Kuwekeza katika Viwanda Tanzania

Ujumbe wa wawekezaji wa makampuni makubwa 15 ya Saudi Arabia utafanya ziara nchini Tanzania tarehe 30 na 31 Januari 2019 kwa madhumuni ya kuangalia fursa ya kuwekeza kwenye viwanda.

Ziar hiyo inatokana na juhudi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Saudi Arabia na wadau wengine  wa kushawishi wafanyabiashara wakubwa kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.

Ujumbe huo wa watu 20, utakapokuwa nchini pamoja na mambo mengine, utashiriki kongamano la biashara litakalofanyika kwenye Hoteli ya New Africa jijini Dar Es Salaam tarehe 30 Januari 2019 kuanzia saa mbili asubuhi. Kongamano hilo litafuatiwa na mazungumzo ya ana kwa ana baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Saudi Arabia.

Kongamano hilo linaloratibiwa na Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) litatoa fursa kwa wafanyabiashara hao kusikiliza mada mbalimbali kuhusu
fursa, vivutio, sheria na kanuni za uwekezaji nchini kutoka taasisi
zinazoratibu masuala ya uwekezaji ikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Ujumbe huo pia unatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi mbalimbali; zikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TANTRADE), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Uwekezaji na Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).

Ziara ya ujumbe huo ni moja ya mikakati ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi na inalenga kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda ili kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe.

Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dodoma.
29 Januari 2019

Monday, January 28, 2019

WAZIRI JAFO ATOA WIKI TATU KWA MHANDISI FRANCIS BAGO


Na.Alex Sonna,Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Seleman Jafo ametoa wiki tatu kwa mhandisi Francis Bago  anayesimamia ujenzi wa kituo cha Afya cha Mkonze Wilaya ya Dodoma, kuhakikisha kituo hicho kimekamirika.


Waziri Jafo ametoa kauli  hiyo leo jijini Dodoma wakati alipokuwa akikagua miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ndani ya Jiji la Dodoma, amesema ndani ya wiki tatu ujenzi wa kituo hicho uwe umekamirika kwani upo nyuma ya wakati.


Amesema huo ni uzembe kuona kituo hicho hakijakamirika kwani kipo Mjini lakini ujenzi wake haujakamirika na unasuasua, wakati vituo vilivyopombali ujenzi wake umekamirika na mgao ulitoka pamoja na wao wapo mwishoni lakini kituo hicho bado sana.


“Nashangaa kuona kituo hiki kipo Mjini kabisa ujenzi wake haujakamilika, wakati huo huo kuna vituo vimekamilika na vipo mbali na fulsa na vifaa vya ujenzi vinapatikana kwa umbali mrefu, kwahiyo huu ni uzembe na naagiza ndani ya wiki tatu ujenzi huu uwe umekamilika,” amesema.


Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni mia nne(400,000,000) kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha Afya, kiasi ambacho kilipelekwa katika Halmashauri nyingi katika kuhakikisha vituo vya Afya vinajengwa.


Vile vile amemtaka mhandisi mshauri wa Jiji la Dodoma kuhakikisha Mradi wa ujenzi wa pakingi ya Magari makubwa kilichopo Nala kuhakikisha kinakamilika kwa wakati ili kuanza kutumika, ameagiza kuhakikisha kinajengwa kwa viwango vinavyotakiwa ili kuepuka kutitia pindi kikianza kutumika.


Waziri Jafo pia ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa Miradi miwili ya Stendi kubwa ya Mabasi na Soko kubwa linalojengwa eneo la Nanenane na kampuni ya ujenzi ya Mohamedi Bulder, na kusisitiza usimamizi thabiti ili miradi hiyo iwe kioo ndani ya Jiji la Dodoma.


Pia amewaagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuanza mapema kupanga namna ya uendeshaji wa miradi hiyo ili iwe kuleta tija kwa Serikali na kuwa chachu ya maendeleo ndani ya Jiji la Dodoma.


Waziri Jafo katika ziara hiyo amekaagua ujenzi wa kituo cha pakingi ya magari makubwa eneo la Nala, ujenzi wa kituo cha Afya Nkonze na ujenzi wa Stendi kubwa ya Mabasi pamoja na Soko kubwa la kimataifa vinavyojengwa eneo la Nanenane ndani ya Jiji la Dodoma.

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA BUNGENI LEO

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Wabunge wa Viti Maalum, Amina Makilagi (katikati) na Fatma Toufiq kwenye viwanja vya Bunge jijjini Dodoma  Januari 28, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Longido Dkt. Stephen Kiruswa, nje ya jengo la utawata Bungeni jijjini Dodoma  Januari 28, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)