SERIKALI YAPELEKA BIL 370 KUKARABATI RELI YA TABORA-MPANDA

 

Na Allan Kitwe, Kaliua


SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetoa kiasi cha shilingi bilioni 379.3 kwa ajili ya kuifanyia maboresho makubwa njia ya reli ya Tabora-Mpanda ili kumaliza kero ya usafiri kwa wananchi.


Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Paschal Kashenshe alipokuwa akitoa taarifa kwa Wajumbe wa  Kamati ya Siasa ya Mkoa waliotembelea mradi huo 


Alisema kuwa mradi huo wa MGS (Meter Gauge Railway) unaanzia Wilaya ya Kaliua kwenda Mpanda ukihusisha uwekaji reli mpya ya zege yenye urefu wa km 210 za njia kuu na km 8 za kupishana.


‘Lengo la mradi huu ni kuongeza uwezo wa reli kupitisha tani 18.5 za mizigo kwa ekseli moja kutoka tani 13.5 za sasa, na kuongeza mwendo kasi kutoka km 30 kwa saa hadi 70’, alieleza.


Alieleza kuwa kwa sasa treni hiyo inatumia muda wa masaa 12 kutoka Tabora kwenda Mpanda na masaa 9 kutoka Kaliua hadi Mpanda lakini utakapokamilika itatumia muda mfupi sana.


‘Tayari tumekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza mataluma ya zege hapa Zugimlole Wilayani Kaliua, mwezi huu mwishoni tunaanza kuzalisha mataluma kwa ajili ya kazi hiyo,’ alidokeza.


Mhandisi Kashenshe alieleza  kuwa lengo la serikali ya awamu ya sita kutoa fedha hizo ni kuhakikisha njia ya reli ya Tabora-Mpanda inakuwa imara na bora zaidi wakati wote.


Akitoa salamu za Chama kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati hiyo baada ya kutembelea mradi huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Jackson Msome aliipongeza serikali kwa kutoa fedha hizo ili kumaliza kero ya wananchi.


Alibainisha kuwa haya ni moja ya matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ili kumaliza kero ya usafiri kwa wananchi wanaotumia reli hiyo.




Comments

Popular posts from this blog

DIWANI WA KEREGE BAGAMOYO, AFIKISHA KILIO CHA WANANCHI DAWASA.

HALMASHAURI YA BAGAMOYO YATENGA SHILINGI BILIONI 2, KWA MWAKA 2026/2027.

DKT. NCHIMBI AWASILI ZANZIBAR, NI MGENI RASMI UZINDUZI WA JENGO LA DAKHALIA SKULI YA HUSNUU MAKAME

TANZANIA KUPATA DOLA MILIONI 41 ZA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI

BAGAMOYO: MJI WA KIHISTORIA UNAONGOJEA MAPINDUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI KUPITIA BANDARI MPYA