PAUL CHACHA APIGA MARUFUKU WANAOFANYA KAMPENI MAPEMA

 

Na Allan Kitwe, Tabora


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wanachama wake wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani au nje ya chama kutofanya kampeni za aina yoyote kabla ya wakati na kuonya kuwa atakayebainika jina lake litaondolewa.


Onyo hilo limetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Oganaizesheni, Paulo Chacha alipokuwa akihutubia umati wa wana CCM, Viongozi na wakazi wa Mkoa wa Tabora katika uwanja wa TBC mjini hapa hivi karibuni.


Amesisitiza kuwa huu sio wakati wa kufanya kampeni, bali ni wakati wa kutumikia wananchi na kujenga chama, hivyo akawataka wale wote wanaoendelea kujipitisha kwa wananchi na kutoa misaada ya kijamii kuacha mara moja tabia hiyo.


‘CCM haikatazi wanachama wake kutoa misaada kwa jamii, ila imeweka utaratibu wa namna bora ya kutoa misaada hiyo ili isionekane kama ni rushwa, kama unataka kusaidia wananchi peleka kwenye Chama, chama kitawagawia’, ameeleza.


Chacha ameelekeza Wenyeviti na Makatibu wa CCM wa Wilaya na Mikoa kutohangaishwa na wanachama wa namna hiyo, bali kila anayepita na kufanya kampeni wakati huu afunguliwe faili ili kile anachokifanya kiwe kwenye rekodi.


Amedokeza kuwa hata kama atashinda kwenye kinyang’anyilo cha kura za maoni chama kitaamua nani anayefaa kupeperusha bendera ya CCM katika nafasi husika, chama hakichagui mtu kwa kutoa rushwa, kinaangalia uwezo wake na usafi wake.


Katibu wa NEC amesisitiza kuwa huu ni wakati wa Wabunge na Madiwani waliochaguliwa na wananchi kutekeleza ahadi walizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, tekelezeni ilani ya uchaguzi kwa vitendo.


CCM ni chama cha watu wote, walio na fedha na wasio na fedha, na kwenye chaguzi hakibagui wagombea wenye fedha na wasio na fedha, wote wanaingia katika kinyang’anyilo kimoja, uwezo wa mtu ndiyo sifa ya kwanza, ameongeza.







Comments

Popular posts from this blog

HALMASHAURI YA BAGAMOYO YATENGA SHILINGI BILIONI 2, KWA MWAKA 2026/2027.

BIL 31 KUKAMILISHA BARABARA YA LAMI KIBONDO MJINI

KAMATI YA BUNGE (PIC) YAITAKA TANAPA KUBORESHA UWEKEZAJI KATIKA HIFADHI ZA TAIFA.

KAMATI YA UCHUMI UJENZI NA MAZINGIRA BAGAMOYO YAKAGUA MIRADI.

SERIKALI YAPELEKA BIL 370 KUKARABATI RELI YA TABORA-MPANDA

WAFANYABIASHARA WASISITIZWA KUTOA NA KUDAI RISITI HALALI

DC NICKSON SIMON: USHIRIKIANO WA SERIKALI NA NGOs NI NGUZO YA MAENDELEO YA WANANCHI

BAKWATA YATANGAZA SIKUKUU YA MAULIDI NI TAREHE 25 AGOSTI 2026