Saturday, August 8, 2026

SERIKALI YAELEKEZA SHILINGI BILIONI 300 KUCHOCHEA TIJA YA KILIMO NCHINI.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye Trekta baada ya uzinduzi wa magari kwa ajili ya Wakala ya Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA) na Matrekta ya vyama vya Ushirika kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane, Kitaifa katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2026.

....................................


Serikali imeongeza uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kupanua upatikanaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na wajasiriamali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza tija katika minyororo ya thamani ya sekta hizo.




Hatua hiyo imebainishwa leo katika Kilele cha Maonesho na Sherehe za Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) mkoani Dodoma, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi bilioni 300 kwa benki saba zitakazotekeleza mpango huo.



Benki zitakazoshiriki ni CRDB, Stanbic, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Tanzania Commercial Bank (TCB), Azania Bank, Benki ya Ushirika, na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).




Mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza rasilimali katika sekta hizo, sambamba na ongezeko la bajeti za kisekta na kuimarisha mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania katika kutoa mikopo ya kutekeleza shughuli za kilimo.




Rais Dkt. Samia amesema Serikali imeongeza mtaji wa benki hiyo kwa shughuli za kilimo, akisisitiza uwekezaji huo uonekane katika tija, uzalishaji, masoko na kipato cha wananchi.




“Tunataka kuona ufanisi huu ukitoa matokeo ya moja kwa moja; tuone mkulima, mvuvi na mfugaji ananufaika kule alipo na anaongeza kipato chake,” amesema Rais Dkt. Samia,

akiongeza kuwa Serikali itaendelea kutafuta masoko ya ndani na nje, huku ikipanua

ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji, uwekezaji na kuongeza thamani.




Katika hatua nyingne, Rais Dkt. Samia ameagiza Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani Kilimo (NAESA) kuimarisha utoaji wa huduma kwa wazalishaji na kukamilisha mifumo ya kidijitali ya kusimamia huduma za ugani nchini.




Vilevile, ameeleza umuhimu wa uzalishaji kuongozwa na taarifa za soko, akitaja tumbaku, kahawa na mazao ya baharini kama mifano ya bidhaa ambazo uzalishaji wake umechochewa na upatikanaji wa taarifa za masoko duniani.




Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema Serikali imeanza maandalizi ya vituo vya kimkakati vya biashara ya mahindi na mpunga katika maeneo manne nchini, ili kuimarisha masoko, uhifadhi na kupunguza upotevu baada ya mavuno.




Ameongeza kuwa Serikali imefikia makubaliano ya kibiashara na Jamhuri ya Sudan Kusini, yatakayowezesha mazao ya kilimo ya Tanzania kuuzwa moja kwa moja nchini humo.




Waziri Chongolo amesema hatua hiyo imefuatia ushiriki wa ujumbe wa Sudan Kusini katika Maonesho ya Nanenane mwaka huu, huku wafanyabiashara zaidi kutoka nchi hiyo wakitarajiwa kushiriki katika maonesho hayo mwaka 2027.




Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema Wizara hiyo

tayari imepokea shilingi bilioni 30 kati ya shilingi bilioni 200 zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana, wanawake na makundi maalum.




Amesema shilingi bilioni saba tayari zimetolewa kwa walengwa, huku shilingi bilioni 23 zikitarajiwa kutolewa kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa shughuli za mifugo na uvuvi.




Akiwasilisha salamu za sekta binafsi, Rais wa Shirikisho la Wakulima Tanzania, Bw. Jitu

Vrajlal Son, amesema ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi utaongeza ufanisi katika kupanga vipaumbele vya kilimo na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




Amesema ushirikiano huo unaweza pia kuharakisha uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea nchini kwa kutumia malighafi zinazopatikana Tanzania, ikiwemo gesi asilia.




Mwenyekiti wa Wabia wa Maendeleo katika Kilimo, Dkt. Nyabenyi Tito Tipo, amesema Maonesho ya Nanenane yameonesha uwezo wa Tanzania kujenga sekta ya kilimo yenye tija, ushindani na ustahimilivu kupitia uwekezaji, sera wezeshi na ushirikiano.




Amesema Wabia wa Maendeleo wataendelea kushirikiana na Serikali kuimarisha uwekezaji katika minyororo ya thamani, teknolojia za kidijitali, kilimo himilivu kwa tabianchi, upatikanaji wa fedha na masoko.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo Maalum kutoka kwa Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo, kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Nanenane Kitaifa, 2026 katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2026.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitembelea banda la Kampuni ya pembejeo za kilimo ya Betaren ya Urusi katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2026.

No comments:

Post a Comment