MANISPAA TABORA KULIPA MIL 27 ZA BODI YA MIKOPO
MANISPAA TABORA KULIPA MIL 27 ZA BODI YA MIKOPO
Na Allan Kitwe, Tabora
HALMASHAURI ya manispaa Tabora imetenga jumla ya shilingi milioni 27 kwa ajili ya kuwalipia watumishi wake waliosoma vyuo vikuu kwa fedha za mkopo wa Bodi ya Elimu ya Juu (HELB) kabla ya kuajiriwa.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya manispaa hiyo Dkt John Pima alipokuwa akitoa taarifa ya hesabu za mwisho (final accounts) kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo
Amesema kuwa halmashauri imetenga kiasi hicho katika bajeti yake ya mwaka huu ili kuwezesha watumishi wake walionufaika na mkopo wa serikali unaotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) kurejesha mikopo yao kwa wakati.
‘Haya ni maelekezo ya serikali kwa waajiri wote nchini kuhakikisha wanatambua watumishi wao waliosoma kwa fedha za mkopo wa bodi hiyo na kurejesha sehemu ya mikopo yao kila mwaka’, ameeleza.
Dkt Pima amedokeza kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kila mwaka ili kuhakikisha kila mtumishi anamaliza marejesho ya mkopo wake ili kuwezesha Bodi hiyo kuendelea kukopesha wanafunzi wengine wenye uhitaji wa mkopo huo wa elimu.
Aidha ameongeza kuwa pia wametenga zaidi ya shilingi milioni 379 kwa ajili ya kulipa madeni ya stahiki mbalimbali za watumishi wa halmashauri hiyo wasio walimu ili kuwaongezea ari ya kufanya kazi kwa weledi mkubwa.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ghullam-Hussein Remtullah amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi na Wakuu wa Divisheni na Vitengo ambayo imepelekea halmashauri hiyo kuendelea kupata hati safi.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya halmashauri hiyo yanachochewa na mshikamano mzuri wa Mkurugenzi, Watalaamu, Watendaji na Madiwani, hivyo akaomba mshikamano huo uendelee ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella amepongeza halmashauri hiyo kwa kuendelea kuandaa vizuri taarifa za hesabu zake za mwaka hali ambayo imepelekea halmashauri kupata hati safi mfululizo.
Akitoa angalizo la mvua za el-nino, DC ameagiza halmashauri na taasisi husika zote kuhakikisha miundombinu ya barabara zote inasafishwa mapema ikiwemo kuzibua mifereji na mitaro ya kupitisha maji ili kuepusha mafuriko mvua zitakapoanza kunyesha.



Comments
Post a Comment