DKT. MWIGULU NCHEMBA AREJESHA TABASAMU KWA WANANCHI WATANO, MGOGORO WA ARDHI MTONI KIZINGA

 

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba,  tarehe 11 Agosti 2026, amerejesha tabasamu kwa

wananchi watano baada ya kufanikisha maridhiano ya mgogoro wa umiliki wa Kiwanja Na. 2013 na 2014, Kitalu “U”, eneo la Mtoni Kizinga, Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, uliodumu kwa miaka 17 kati ya mfanyabiashara Hersi Warsame Mohamed na wananchi hao.


Katika mgogoro huo, wananchi hao wakiongozwa na Bw. Ivan Kihiyo, walimwandikia barua Mheshimiwa Waziri Mkuu wakilalamika kuwa mfanyabiashara Hersi Warsame Mohamed amejimilikisha eneo lao kinyume cha sheria. Wananchi hao walimuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua mgogoro huo.


Timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotumwa na Waziri Mkuu kutatua mgogoro huo, ikiongozwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Msaidizi wa Waziri Mkuu – Mahusiano, Asasi za Kiraia na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bw. Tryphone Mkolokoti, na Katibu wake ambaye pia ni Msaidizi wa Waziri Mkuu – Masuala ya Ardhi, Bw. Senso Magessa, ilifanikiwa kufanikisha maridhiano hayo kwa kuzingatia taarifa ya uchunguzi wa mgogoro huo iliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), hukumu ya Mahakama katika kesi iliyofunguliwa na wananchi hao ambayo Bw. Hersi Warsame Mohamed alishinda, pamoja na maelezo ya Maafisa Ardhi kutoka Manispaa ya Temeke walioshiriki katika

mchakato wa maridhiano.


Utiaji saini wa makubaliano ya maridhiano hayo ulifanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu,

Magogoni, jijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na Walaam wa Ardhi kutoka Manispaa ya Temeke, Bw. Salim Shedafa na Bw. Salim Urembo, pamoja na Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.


Pande zote mbili zilimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa utaratibu mzuri unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kutatua migogoro ya wananchi kwa njia ya mazungumzo na maridhiano.


Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, kiongozi wa wananchi hao, Bw. Ivan Kihiyo, alisema: “Tumefikia maridhiano haya kwa akili zetu wenyewe, bila kushurutishwa, na tumekubaliana kulimaliza suala hili kwa amani. Wenzetu hawakushurutishwa na sisi hatukushurutishwa.”


Naye Msemaji wa familia ya Bw. Hersi, Yassin Hersi Warsame, alimshukuru Mungu kwa mgogoro huo kumalizika kwa njia ya maridhiano. Alisema familia itaendelea na uwekezaji wake katika eneo hilo na kuchangia katika ujenzi wa Taifa la Tanzania bila bughudha.


Waziri Mkuu ameweka utaratibu wa kutatua baadhi ya migogoro mbalimbali ya wananchi

inayomfikia kupitia mikutano ya hadhara na kwa njia ya barua, kwa kutumia Kamati yake ya Maridhiano, ambayo imeendelea kutatua migogoro mbalimbali kadiri inavyoagizwa na Waziri Mkuu.







Comments

Popular posts from this blog

DIWANI WA KEREGE BAGAMOYO, AFIKISHA KILIO CHA WANANCHI DAWASA.

DKT. NCHIMBI AWASILI ZANZIBAR, NI MGENI RASMI UZINDUZI WA JENGO LA DAKHALIA SKULI YA HUSNUU MAKAME

BAGAMOYO: MJI WA KIHISTORIA UNAONGOJEA MAPINDUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI KUPITIA BANDARI MPYA

TANZANIA KUPATA DOLA MILIONI 41 ZA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI

KIKWETE ATEMBELEA BANDA LA HALMASHAURI YA MJI BAGAMOYO NANENANE