Saturday, August 8, 2026

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI IBADA YA MISA TAKATIFU YA JUMUIYA YA URU SEMINARI

 


MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI IBADA YA MISA TAKATIFU YA JUMUIYA YA URU SEMINARI.


ASISITIZA SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA TAASISI ZA DINI KATIKA MAENDELEO YA TAIFA HUSUSANI SEKTA YA AFYA NA ELIMU



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Taasisi za Dini ambazo kwa namna ya pekee zimekuwa zikishiriki katika kutoa mchango kwenye sekta za Afya na Elimu hapa nchini.

 



Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu Maalum ya Wanajumuiya wa Uru Seminari, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kristo Mchungaji Mwema – Tabata Kimanga Jijini Dar es Salaam. 



Amesema kwa miaka mingi na kwa asilimia kubwa Taasisi za dini zimechangia katika utoaji wa huduma za elimu na afya, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi hizo ili kufanikiwa zaidi katika kulijenga Taifa.



 

Makamu wa Rais amesema Malezi yanayotolewa katika Taasisi za elimu za dini ikiwemo Shule ya Uru Seminari ambayo husisitiza Sala, Kazi na Masomo yanapaswa kutiliwa mkazo katika malezi ya vijana wa sasa. 



Amesema vijana watakavyoweza kumjua Mungu, kufanya kazi kwa bidii pamoja na kupata elimu wataweza kulijenga vema Taifa kupitia ujuzi na hivyo kuepusha tabia za kupata kipato kupitia njia zisizo sahihi.



 

Makamu wa Rais amewashukuru, walimu, walezi na wanafunzi waliopata elimu Uru Seminari kwa ushirikiano na malezi mazuri ambayo yalifundisha kumtumikia Mungu pamoja na Wanadamu.

 



Amewasihi Wanajumuiya ya Uru Seminari kuendeleza umoja na kuhakikisha unakuwa wenye tija kwa Taifa, pamoja na kuendelea kuiombea nchi na Viongozi wake.

 



Ibada ya Misa Takatifu ya Wanajumuiya wa Uru Seminari, imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, Mhashamu Joseph Mlola.

 



Akitoa mahubiri kwa Wanajumuiya wa Uru Seminari , Askofu Mlola amewasihi kukumbuka wito muhimu walionao wa kupeleka tunu njema ya Maisha ya kiimani kuishi kwa kumpendeza Mungu pamoja na wanadamu. 



Amesema ni muhimu kuwa mstari wa mbele kupeleka matumaini, ukweli, amani na haki.

 



Pia, Askofu Mlola amewasihi kuhakikisha uwepo wa kila mwanajumuiya wa Uru Seminari analeta upendo na matumaini, kwa kutambua huo ni wito kwao waliolelewa na kufundishwa katika malezi na maadili mema.

 

Uru Seminari ni Shule inayomilikiwa na Shirika la Mitume wa Yesu chini ya Kanisa Katoliki  Jimbo Moshi Mkoani Kilimanjaro.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

08 Agosti 2026

Dar es Salaam.








No comments:

Post a Comment