CCM TABORA YATOA MAAGIZO KWA BODI YA TUMBAKU KUMALIZA KERO ZA WAKULIMA
Na Allan Kitwe, Tabora
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora kimeitaka Bodi ya Tumbaku nchini (TTB) kuja na mikakati thabiti itakayosaidia kumaliza kero za wakulima wa zao hilo Mkoani humo na Mikoa mingine hapa nchini.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Said Juma Nkumba alipokuwa akizungumza kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kilichofanyika jana Wilayani Kaliua Mkoani hapa.
Amesema kuwa zao la tumbaku ni zao muhimu sana kwa uchumi wa wakazi wa Mkoa huo na Mikoa mingine, lakini limekuwa likikabiliwa na changamoto kadha wa kadha hali ambayo imekuwa ikilalamikiwa mno na wananchi.
'Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali ambazo imekuwa ikichukua ili kuhakikisha kilimo kinaboreshwa na masoko ya uhakika yanapatikana’, ameeleza.
Komredi Nkumba amedokeza kuwa CCM inajivunia mafanikio makubwa ambayo yameendelea kupatikana katika sekta ya kilimo na sekta nyingine na kuongeza kuwa kero wanazokumbana nazo wakulima wa zao hili zinawaumiza.
‘Katika kikao hiki tumemwalika Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku nchini (TTB) ili atueleze jinsi walivyojipanga kumaliza kero za tumbaku, mkulima anapaswa kujua bei ya soko kabla ya kuanza msimu mpya wa kilimo’, amesema.
Ilani ya uchaguzi ya CCM inaeleza bayana kuwa shughuli za wakulima zitaendelea kuboreshwa ili kuwakwamua kiuchumi, hivyo changamoto za tumbaku zinapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, ameongeza Nkumba.
Akifafanua hoja zilizotolewa, Mkurugenzi wa TTB Stanley Nozya ameipongeza CCM na Uongozi wa Mkoa kwa kuialika Bodi hiyo ili ije kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu zao la tumbaku.
Amekiri kuwepo changamoto kadhaa kwenye masoko ya zao hilo hali ambayo ameeleza kuwa inasababishwa na mambo kadhaa ikiwemo hali ya soko la dunia, uchache wa wanunuzi wenye uwezo mkubwa na ubora wa tumbaku ya wakulima.
‘Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Bodi ya Tumbaku tumeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kumaliza kero za wakulima wa tumbaku na kupanua wigo wa masoko ili kuhakikisha tumbaku yote inayozalishwa inanunuliwa’, ameeleza.
Nozya amepongeza wakulima wa Mkoa huo kwa kuongoza kwa uzalishaji wa tumbaku nchini ila akaeleza kusikitishwa na tabia ya baadhi yao kuchanganya tumbaku safi na chafu hali inayopelekea kuuza kwa bei ndogo au kukataliwa kabisa.
Katika msimu ujao tuna habari njema kwa wakulima wa tumbaku, muda sio mrefu tutatambulisha wanunuzi wapya 2 wakubwa kutoka nje, ambao wana uwezo wa kununua tumbaku nyingi zaidi, hilo linashughulikiwa na serikali,’ amedokeza.
Ameeleza kuwa TTB itaandaa mkutano maalumu wa wadau wa tumbaku na wanahabari ili kupokea kero, maoni na ushauri mbalimbali utakaosaidia kuboresha kilimo cha zao hilo na kuinua maisha ya wakulima kwa ujumla.





Comments
Post a Comment