DC NICKSON SIMON: USHIRIKIANO WA SERIKALI NA NGOs NI NGUZO YA MAENDELEO YA WANANCHI

 

KIBAHA – Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, amezitaka Asasi Zisizo za Kiserikali (NGOs) wilayani humo kuimarisha ushirikiano na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuongeza tija na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.


Akifungua kikao cha mashauriano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na wawakilishi wa NGOs kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, DC. Nickson alisema Serikali na NGOs zina lengo moja la kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo ni muhimu shughuli na miradi inayotekelezwa iwe na mshikamano na kuendana na vipaumbele vya taifa.


Alieleza kuwa ushirikiano huo unaonekana katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, ambapo Serikali na NGOs zote zinatekeleza miradi ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.



Aliongeza kuwa hali hiyo pia ipo katika sekta za afya, mazingira, haki za binadamu pamoja na uwezeshaji wa makundi maalumu.


Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya aliainisha maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele na NGOs kwa kuzingatia mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo. Maeneo hayo ni pamoja na matumizi ya majukwaa ya kidijitali (digital platforms), uwezeshaji wa vijana na ajira, pamoja na uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi.


Mhe. Nickson pia alishiriki uzoefu wake kuhusu mbinu za kutafuta na kupata ufadhili kwa taasisi za maendeleo. Alizitaka NGOs kujijenga na kujipanga vizuri ili kuvutia wafadhili kwa kuwa na maandiko na mawasilisho yenye kuonyesha mahitaji halisi ya jamii kwa usahihi.


“Ni muhimu kuwa mahususi katika kuandaa miradi na mapendekezo ya ufadhili. Epukeni kuwa wa jumla sana; elezeni changamoto, malengo na matokeo yanayotarajiwa kwa uwazi ili kuongeza uwezekano wa kupata fedha,” alisema.


Aidha, aliwahimiza viongozi wa NGOs kuanza kutumia fursa za wafadhili wa ndani ya nchi badala ya kutegemea wafadhili wa nje pekee, akibainisha kuwa rasilimali za ndani zinaweza kuwa chanzo muhimu cha kuendeleza miradi yenye manufaa kwa jamii kwa muda mrefu.


Kikao hicho kilitoa fursa kwa Serikali na NGOs kubadilishana mawazo kuhusu namna bora ya kuimarisha ushirikiano na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya Wilaya ya Kibaha.





Comments

Popular posts from this blog

DIWANI WA KEREGE BAGAMOYO, AFIKISHA KILIO CHA WANANCHI DAWASA.

DKT. NCHIMBI AWASILI ZANZIBAR, NI MGENI RASMI UZINDUZI WA JENGO LA DAKHALIA SKULI YA HUSNUU MAKAME

BAGAMOYO: MJI WA KIHISTORIA UNAONGOJEA MAPINDUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI KUPITIA BANDARI MPYA

TANZANIA KUPATA DOLA MILIONI 41 ZA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI

KIKWETE ATEMBELEA BANDA LA HALMASHAURI YA MJI BAGAMOYO NANENANE

VERONICA MREMA WA TANZANIA AINGIA SITA BORA TUZO ZA ISU ELIHLE 2026 AFRIKA