SAMIA AKUTANA NA MAASKOFU WA KATOLIKI, WAZUNGUMZA AMANI NA MUSTAKABALI WA TAIFA
Na Albert Kawogo
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini kupitia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), katika hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na viongozi wa dini.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo, Agosti 10, 2026, katika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, ambapo viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya kitaifa, yakiwemo siasa, imani, amani, mshikamano na maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, mkutano huo umeangazia pia umuhimu wa kuendelea kuimarisha amani na mshikamano wa Taifa, pamoja na kujenga mustakabali wenye ustawi kwa Watanzania.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili nafasi ya madhehebu ya dini na viongozi wake katika kujenga jamii yenye maadili mema, uwajibikaji na mshikamano, sambamba na kuchangia juhudi za maendeleo endelevu ya Taifa.
Rais Samia amewashukuru Maaskofu hao kwa kuona umuhimu wa kukutana naye na kujadili masuala yenye tija kwa Taifa, akisisitiza umuhimu wa mazungumzo na mashauriano katika kujenga uelewano na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Aidha, Rais Samia amewahakikishia viongozi hao dhamira yake ya kuendeleza utamaduni wa kushauriana na kushirikisha viongozi wa dini pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii katika kujadili na kutafuta suluhisho la masuala muhimu yanayolihusu Taifa.
Mkutano huo unakuja wakati ambapo ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini unaendelea kuwa sehemu muhimu katika juhudi za kuimarisha amani, maadili, mshikamano na maendeleo ya Tanzania.

Comments
Post a Comment