WAFANYABIASHARA WASISITIZWA KUTOA NA KUDAI RISITI HALALI
13 Agosti 2026, KAGERA
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera imeendelea kuwakumbusha wafanyabiashara umuhimu wa kutoa na kudai risiti halali za mashine za kielektroniki (EFD) kila wanapofanya mauzo, huku ikisisitiza kuwa matumizi ya risiti bandia ni kinyume cha sheria.
Akizungumza katika zoezi la Alhamisi ya Mlipakodi, Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, CPA Joseph Mtalemwa, amewataka wafanyabiashara kuzingatia sheria na taratibu za kodi kwa kuhakikisha wanatoa risiti halali kwa wateja wao na kudai risiti wanapofanya manunuzi.
CPA Mtalemwa amesema utoaji wa risiti bandia ni kosa kisheria na umewataka wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao wa kikodi kwa uaminifu, hatua ambayo itasaidia kuimarisha uwazi katika biashara na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Katika zoezi hilo, wafanyabiashara walipata pia fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za biashara pamoja na kutoa maoni na mapendekezo kuhusu maeneo wanayoona yanahitaji kuboreshwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wameipongeza TRA kwa kuendelea kuwafikia, kuwasikiliza na kuwajali kupitia programu za mawasiliano na ushirikishwaji. Wamesisitiza kuwa zoezi hilo liendelee ili kuwezesha mawasiliano ya karibu kati ya TRA na wafanyabiashara, pamoja na kujenga uelewa zaidi kuhusu masuala ya kodi.




Comments
Post a Comment