SAMIA: MAULID ITUKUMBUSHE KUISHI KWA UPENDO NA AMANI

 

SAMIA: MAULID ITUKUMBUSHE KUISHI KWA UPENDO NA AMANI


Na Rashid Mtagaluka


DAR ES SALAAM: 


Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kutumia maadhimisho ya Maulidi kutafakari maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W) na kujifunza misingi ya upendo, wema na amani.


Ujumbe huo wa Rais Samia umetolewa leo, Agosti 25, 2026, na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyemwakilisha Rais katika Baraza la Maulidi lililofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), jijini Dar es Salaam.


Katika ujumbe huo, Rais Samia amesema maadhimisho ya mazazi ya Mtume Muhammad yanapaswa kuwa fursa ya kuwakumbusha waumini umuhimu wa kuishi kwa upendo, amani na kutendeana mema.


Amesema kutafakari maisha ya Mtume Muhammad kutawasaidia Watanzania kuona uzuri wa mafundisho yake na kuyaweka katika maisha ya kila siku.


Akizungumza kwa niaba ya Rais, Dkt. Nchemba amesema serikali imedhamiria kuendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kujenga jamii yenye maadili, akisisitiza umuhimu wa malezi ya watoto na vijana.


Amesema mazingira ya sasa yameleta changamoto mpya katika malezi, huku watoto wa kiume akiwataja kuwa miongoni mwa wanaokabili hatari kubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa zamani.


“Watoto wakifundishwa vema malezi mazuri, hata wakikua hawataacha,” amesema Dkt. Nchemba, akisisitiza kuwa malezi si jukumu la wazazi pekee bali la jamii nzima.

Amegusa pia matumizi ya mitandao ya kijamii, akimpongeza Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakari Zubeir Bin Ally Mbwana, kwa kuendelea kuhimiza matumizi sahihi ya mitandao miongoni mwa vijana.


Katika eneo la amani na umoja wa kitaifa, Dkt. Nchemba amesema amani inapaswa kuendelea kuwa msingi wa maendeleo ya Tanzania, ikiwamo kuvutia uwekezaji.


Amesisitiza umuhimu wa kuheshimu Katiba, haki na wajibu wa kila mwananchi, akisema migogoro ya kidini haina mshindi na kwamba Watanzania wanapaswa kujenga utamaduni wa kuvumiliana na kuheshimiana.


Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakari Zubeir Bin Ally Mbwana, amewataka viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza majukumu yao badala ya kusubiri kuondolewa madarakani.


Mufti Zubeir amesema viongozi hawapaswi kuwa “wachungu mno mpaka wakatemwa”, wala kuwa “watamu mno mpaka wakalambwa”, akisisitiza kuwa uongozi ni dhamana inayopaswa kuonekana kupitia kazi na matokeo.


Amesema kiongozi hapaswi kushikilia nafasi kwa ajili ya nafasi yenyewe, bali kutumia dhamana aliyopewa kuwatumikia Waislamu na kuendeleza taasisi.


Kauli hiyo imekuja wakati BAKWATA ikiwa imekamilisha  mchakato wa kupata uongozi wake katika ngazi za msikiti, kata, wilaya, mkoa na Taifa, huku viongozi wapya wakichaguliwa kushika nafasi mbalimbali.


Dkt. Nchemba amewapongeza waliochaguliwa na kuwataka ambao hawakupata nafasi hizo kutokuwa na “nongwa”, akisema mabadiliko ya uongozi ni jambo la kawaida katika taasisi.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Nchemba ameahidi  kuchangia safari ya mahujaji wa mwaka huu kwa kuwapeleka kati ya mahujaji watano hadi 10, kutegemea hali ya uchumi.


Baraza hilo limefanyika ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Maulidi, likiwakutanisha viongozi wa Serikali, viongozi wa dini na waumini kutoka maeneo mbalimbali.





Comments

Popular posts from this blog

LISU AKUTWA NA KESI YA KUJIBU.

BAKWATA YATANGAZA SIKUKUU YA MAULIDI NI TAREHE 25 AGOSTI 2026

WATU 16 JELA KWA MAKOSA YA WIZI, UBAKAJI.

SHAIBU NDEMANGA, AFUNGUA MAFUNZO YA JESHI LA AKIBA.

RAIS, DKT. SAMIA, ARIDHIA KUJIUZULU MAKAMU WA RAIS.

NEEMA YAWASHUKIA WAKULIMA WA TUMBAKU

KISARAWE YAJA NA SULUHU MAHITAJI YA BARUTI, VILIPUZI NCHINI