KIKWETE: KARAKANA ZA SHULE ZITUMIKE KUKUZA UBUNIFU NA UJUZI WA VIJANA

 

Na Albert Kawogo, BAGAMOYO:


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amezitaka shule kutumia ipasavyo karakana zinazojengwa katika utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi, kukuza vipaji na kujenga uwezo wa kujiajiri.


Kikwete amesema karakana hizo hazipaswi kufunguliwa au kutumika wakati wa ziara za viongozi pekee, bali zinapaswa kuwa sehemu muhimu ya mazingira ya kujifunzia na kuwaandaa vijana kwa maisha ya baadaye.


Amesema Taifa haliwezi kujengwa kwa kutegemea vyeti pekee, bali linahitaji watu wenye uwezo wa kutumia maarifa yao kutatua changamoto na kubadilisha changamoto hizo kuwa fursa za kiuchumi.


“Endapo karakana hizi zitatumika vizuri, zitaibua fani na vipaji vya watoto na kuwafanya kuwa wabunifu, jambo ambalo litawasaidia kujiajiri na kuajirika katika maeneo mbalimbali hapa nchini,” amesema Kikwete.


Waziri huyo ameyasema hayo Agosti 15 alipokuwa akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Shule za Shajar, inayomiliki Shule za Msingi na Sekondari za Baobab pamoja na Chuo cha Afya na Ufundi na zahanati.


Kikwete, ambaye alimwakilisha Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, pia ameuagiza uongozi wa taasisi hiyo kuhakikisha unasajili kazi za ubunifu zinazofanywa na wanafunzi ili kulinda haki zao za umiliki na kuzuia kazi hizo kuibiwa au kutumiwa na watu wengine bila idhini.


Aidha, ameitaka Baobab Vocational Center kuwa daraja la kuwawezesha vijana kutoka katika hatua ya kuwa na vipaji hadi kufikia uzalishaji, kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi pamoja na ujasiriamali, usimamizi wa fedha na namna ya kutafuta masoko ya bidhaa na huduma wanazozalisha.


Naye  Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, ameipongeza Taasisi ya Shule za Shajar kwa mchango wake katika kuwaandaa vijana kujiajiri kwa kutumia ujuzi na ubunifu wanaoupata kupitia elimu..


Ndemanga amesema Wilaya ya Bagamoyo hivi karibuni itaandaa maonyesho yatakayoshirikisha shule na taasisi zinazotoa elimu ya amali, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuona uwezo wa watoto katika taaluma mbalimbali pamoja na kazi za ubunifu wanazozalisha..


Kwa upande wake Kamishna wa Elimu, Lyambwene Mutahabwa, amewataka wananchi kushirikiana katika kuwalinda watoto na kuhakikisha wanakulia katika mazingira bora na salama yatakayowawezesha kupata elimu na kukuza vipaji vyao..


Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Shule za Shajar, Shani Swai, ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi, akisema hatua hiyo imeendelea kuchangia ukuaji wa sekta ya elimu nchini.


Comments

Popular posts from this blog

DIWANI WA KEREGE BAGAMOYO, AFIKISHA KILIO CHA WANANCHI DAWASA.

HALMASHAURI YA BAGAMOYO YATENGA SHILINGI BILIONI 2, KWA MWAKA 2026/2027.

DKT. NCHIMBI AWASILI ZANZIBAR, NI MGENI RASMI UZINDUZI WA JENGO LA DAKHALIA SKULI YA HUSNUU MAKAME

BAGAMOYO: MJI WA KIHISTORIA UNAONGOJEA MAPINDUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI KUPITIA BANDARI MPYA

TANZANIA KUPATA DOLA MILIONI 41 ZA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI

BIL 31 KUKAMILISHA BARABARA YA LAMI KIBONDO MJINI