Na Karama Kenyunko
CHAMA cha ACT- Wazalendo kupitia bodi yake ya
dhamini, wamewasilisha maombi ya kujiunga katika kesi ya kikatiba
iliyofunguliwa na mkulima Dezydelius Patrick Mgoya, ambaye anahoji kuwepo kwa
kikomo cha urais nchini.
Maombi hayo yamebainishwa leo Septemba 30, 2019 na
Jaji Kiongozi wa mahakama hiyo, Dk Eliezer Feleshi, wakati kesi hiyo ilipokuja
kwa ajili ya kutajwa na maelekezo maalumu ya namna ya usikilizwaji wa pingamizi
la awali la Seriali dhidi ya kesi ji Kiongozi Dk Feleshi ndiye kiongozi wa jopo
la majaji wanaosikiliza kesi hiyo. Wengine katika kesi hiyo ni Dk. Benhajj
Masoud na Seif Kulita.
Katika maombi hayo, ACT inayowakilishwa na kampuni
ya uwakili ya Law Guards Advocates wamewasilisha maombi hayo chini ya hati ya
dharura, wakiomba maombi yao yasikilizwe haraka.
Kufuatia maombi hayo, mahakama imesimamisha
usikilizwaji wa kesi ya msingi na kuamua kusikiliza kwanza maombi hayo ya
ACT-Wazalendo.
Jaji Feleshi ambae anaongoza jopo la majaji watau
wakiwemo Dk. Benhajj Masoud na Seif Kulita amesema, maombi hayo ya ACT- Wazalendo
yatasikilizwa na jaji mmoja ambaye atalitaarifu jopo hilo kuhusu uamuzi
utakaofikiwa na kesi hiyo sasa itatajwa Oktoba 25 kwa ajili ya maelekezo
muhimu.
Wakili wa ACT- Wazalendo, Jebra Kambole ameeleza
kuwa maombi ya wateja wake yamepangwa kusikilizwa na jaji Benhajj na kwamba
yamepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza keshokutwa, Jumatano, Oktoba 2, 2019.
Katika maombi hayo pamoja na mambo mengine, chama
hicho kinadai kuwa ikiwa uamuzi wa kesi hiyo utapitishwa bila wao kushirikishwa
kitaathirika na kwamba kina haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Mkulima huyo mkazi wa Mbezi Beach, jijini Dar es
Salaam, Patrick Dezydelius Mgoya amefungua kesi hiyo Mahakama Kuu, Masjala Kuu
dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiiomba mahakama hiyo itoe tafsiri
sahihi ya ibara ya katiba inayoweka ukomo huo wa urais.
Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo namba 19
ya mwaka 2019 Mgoya anahoji Ibara ya 40 (2) ya Katiba ambayo inaweka ukomo wa
mihula miwili tu ya miaka mitano mitano (10) ya uongozi katika nafasi hiyo ya
urais.
Hivyo anaiomba mahakama hiyo itoe tamko na tafsiri
ya maana sahihi na athari za masharti ya ibara hiyo.
Pia anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana dhahiri
ya masharti ya Ibara ya 42(2) ya Katiba, kwa kuhusianisha na na masharti ya
Ibara za 13, 21 na 22 za Katibahiyo.
Vilevile anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana ya
Ibara hiyo ya 40(2) kwa kuhusianisha na Ibara ya 39 ya Katiba.
Katika hati yake ya kiapo kinachounga mkono kesi
hiyo, Mgoya anadai kuwa lakini Ibara ya 40(2) ya Katiba inaweka ukomo wa muda
wa mtu kuchaguliwa kuwa rais, kwamba mtu hawezi kuchaguli zaidi ya mara mbili
kushikilia wadhifa wa uraisi
Hivyo anadai kuwa masharti ya ibara hiyo ya 40(2)
yanakiuka haki za kikatiba za Ibara za 13, 21 na 22(2) za Katiba hiyohiyo kwa
kutoa mihula miwili tu ya raia kuchaguliwa kuwa rais kwa ukomo wa miaka 10 tu.
Mgoya anadai kuwa ukomo uliowekwa chini ya Ibara ya
40(2) ya Katiba yanakinzana na haki ya kikatiba ya uhuru wa kushiriki katika
shughuli za umma kwa kuchagua au kuchaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na usawa mbele ya sheria chini ya Ibara ya 21 na 13
CHANZO, MICHUZI BLOG.
No comments:
Post a Comment