Tuesday, September 17, 2019

RC. PWANI AMFAGILIA MKURUGENZI WA AZANIA BANK KWA KUUNGA MKONO SERA YA VIWANDA.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo kulia akisalimiana na kumpongeza Mkurugenzi wa Benki ya Azania, Charles Itembe kwa kusapoti masuala ya uwekezaji  mara baada ya kumalizika kwa halfa ya uwekaji wa jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio kilichopo katika kata ya Pangani Wilayani Kibaha.
.......................................
NA MWANDISHI WETU, PWANI.

WAWEKEZAJI wa  sekta ya viwanda wametakiwa kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu zote za kazi na kuachana na vitendo vya kuvunja sheria za nchi kwa kuamua kuwanyanyasa wafanyakazi wao kwa kuwanyima haki zao za msingi ikiwemo kuwapatia huduma ya matibabu, pamoja na kuwapatia maslahi yao kama inavyotakiwa bila ya  kuwa na vitisho vyovyote ili kutimiza azma ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu  wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja  kwa ajili ya uwekeji wa  jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengenezea vifungashio (WANDE PRINTING)  vitumikavyo katika sekta ya chakula, kilimo, viwanda, afya,  ujenzi pamoja na kiwanda  ambacho kinajengwa katika  eneo la  kata ya Pangani Wilayani Kibaha na kuwaasa watendaji na mamlaka zinazohusika kuwapa ushirikiano wa kutosha wawekezaji hao bila ya ubaguzi na ubinafsi  wowote.

Ndikilo alisema kwamba serikali ya awamu ya tano lengo lake kubwa ni kuendelea kushirikiana na wawekezaji mbali mbali wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Jojn Pombe Magufuli, hivyo wafanyakazi wanatakiwa kupewa haki zao stahiki bila ya kuonewa hasa katika suala la vitendea kazi pindi wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Katika Mkoa wa Pwani kwanza nashukuru kwa sasa tunaendelea kushirikiana na wawekezaji wazawa ambao wamekuwa na nia ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya viwanda katika maeneo mbali mbali.

"Lakini kila siku Rai yangu kubwa ni kuwapa haki zao zote waafanyakazi kwani wao ndio wapo mstari wa mbele katika kuzalisha bidhaa, kwa hivyo katika hili naomba sana kwa wawekezaji kuliangalia kwa jicho la tatu.” alisema Ndikilo.

Aidha Mkuu huyo aliipongeza Benki ya Azania kwa kuweza kuonyesha uzalendo kwa kushirikiana bega kwa bega na serikali ya awamu ya tano katika kutoa msaada wa kuwawezesha mikopo wawekezaji ikiwemo kiwanda hicho  kwa lengo la kuweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi kupitia sekta ya viwanda.


Kwa upande wake mmoja wa wawekezaji wazawa katika kiwanda hicho John Obach akisoma risala kwa mgeni rasmi kwa niaba viongozi wenzake amebainisha kuwa ujenzi wa mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.6 na kwamba wanatarajia kutoa ajira zaidi ya 300 ambazo zitaweza kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi na kuondokana na wimbi la umasikini.

Naye  Mkurugenzi wa Azania Benki Charles   Itembe ambao ndio wamewezesha kwa kiasi kikubwa  ujenzi wa mradi huo wa kiwanda  amesema kwamba lengo lao kubwa ni kuunga mkono  sera ya Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwa na uchumi wa viwanda na kuahidi kuendelea kushirikiana na wawekezaji wengine katika kuinua sekta ya viwanda.


“Sisi kama  taasisi ya kifedha Azania Benki nia na madhubmuni yetu makubwa ni kuhakikisha tunaaunga sera ya Rais wetu wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwa na Tanzania ya viwanda, kwa hivyo ndio maana tumeamua kuwawezesha wenzetu wa kiwanda hiki cha kutengenezea vifungashio ili kuleta mapinduzi ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Aliongeza kwa kusema kuwa, kwa sasa wataendelea kutoa misaada kwa wadau wa maendeleo pamoja na serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata fursa mbali mbali za ajira kupitia miradi ya ujenzi ywa viwanda ambavyo vinajengwa katika maeneo tofauti lengo ikiwa ni kuondokana na wimbi la umasikini na kujikwamua kiuchumi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani  Mhandisi Evarist Ndikilo wa kulia akipeana mkono na Mwenyekiti wa makampuni ya Global Packaging na Wande Printing Joseph Wasonga  mara baada ya kumalizika kwa zoezi la uwekaji wa jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengenezea vifungashio kilichojengwa Wilayani Kibaha.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akikagua moja ya bidhaa ambazo zinazalishwa katika kiwanda cha Wande Printing ambacho kinatengeneza vifungashio wakati alipofanya ziara yake ya kikazi kwa ajili ya uwekaji wa jiwe la msingi katika kuwanda hicho. 
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarit Ndikilo  akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbali mbali wa serikali, viongozi wa kiwanda hicho pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo ikiwemo Mkurugenzi wa benki ya Azania kulia kwake Charles Itembe.
  
 

No comments:

Post a Comment