Friday, September 27, 2019

BAGAMOYO WATAKIWA KUJIANDIKISHA

Na Omary Mngindo, Bagamoyo.


WANANCHI Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, ikiwa ni kuelekea kwenye chaguzi za viongozi wa serikali za vijiji na vitongoji.


Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa uchaguzi wilayani hapa Malboard Kapinga, akizungumza na wadau wa zoezi hilo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali, lililozitaka halmashauri zote kuitisha vikao na wadau kuzungumzia mchakato huo.


"Halmashauri ya wilaya kwa Mamlaka tuliyopewa chini ya kanuni 9 (1) na (2) ya uchaguzi wa Wenyeviti, tangazo la serikali namba 373 la tarehe 26/4/2019 pamoja na kanuni zake, hapa Bagamoyo tayari zoezi la uandikishwaji limeshaanza," alisema Kapinga.


Aliongeza kwamba uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji katika mamlaka za miji midogo kanuni ya 08 (1) na (2), tangazo la serikali namba 371 la tarehe 26/4/2019, anawatangazia wananchi kuwa Nov 24 mwaka huu kutafanyika uchaguzi wa serikali za mitaa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Fatuma Latu amesema kuwa, wameitisha kikao hicho ikiwa ni kutekeleza agizo la serikali linalowataka kuwa na vikao vitakavyohusisha wadau kuelekea kwenye chaguzi zijazo.


"Niwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi, kikao chetu kimezingatia maelekezo yaliyotolewa na serikali inayozitaka halmashauri zote nchini kuitisha vikao vitakavyojadili masuala muhimu wakati tunaelekea kwenye chaguzi," alisema Latu.


Wakichangia mada kwenye kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani humo Mathei Torongey amelalamikia hujuma alizofanyiwa na Mtendaji kijiji cha Mkenge, aliyewavamia wakiwa wanapeana maelekezo kuhusiana na kikao hicho.


"Nimefurahi kuwaona viongozi wa dini mnaounda Kamati ya amani mko hapa, tunawataka mtoe matamko yanayohusiana na kukemea dalili za uvunjifu wa amani, kitendo alichokifanya Mtendaji kinaashiria uvunjifu wa amani," alisema Torongey.


Nae Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mohamed Usinga diwani wa Kata ya Yombo amekumbushia fujo alizofanyiwa na wafuasi wa CHADEMA kwenye chaguzi zilizopita, hatua aliyoielezea imechangiwa na viongozi wao.

No comments:

Post a Comment