Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akibadilishana mawazo na
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti mara baada ya kuwasili
ofisini kwake kuanza ziara ya kanda ya ziwa.
Naibu Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akipewa maelezo ya ranchi za
Mabale, Kagoma na Kikulula zilizopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera na Kaimu
Meneja Mkuu wa NARCO Prof. Phillemon Wambura.
..............................
Serikali imesema itahakikisha katika kipindi cha miezi
mitatu ijayo changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi kwenye soko la nyama nje
ya nchi zinatatuliwa ili kuhakikisha wafugaji wananufaika kupitia mifugo yao
kwenye soko la nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega
amesema hayo katika Ranchi ya Kikulula iliyopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera
wakati akizungumza na wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo, ikiwa
ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo, ambapo
amesema baadhi ya masoko nje ya nchi hushindwa kununua nyama kutoka Tanzania
kwa madai yasiyo sahihi kuwa mifugo iliyopo nchini ina maradhi.
Akizungumza na wawekezaji takriban 33 waliopewa
vitalu katika ranchi ya Kikulula iliyopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, Naibu
Waziri Ulega amesema katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ni lazima vikwazo
vilivyopo katika soko la nyama nje ya nchi viwe vimetatuliwa kwa wawekezaji
kwenye vitalu kuwa na mipango maalum ya ufugaji ili wakaguzi kutoka nje ya nchi
wakija kukagua ubora wa mifugo nchini wapate taarifa sahihi itakayowezesha
mifugo na nyama itokanayo na mifugo hiyo ipate soko nje ya nchi kwa kuwa na
afya bora.
Aidha Waziri Ulega amesema Ranchi ya Kikulula
lazima iendelezwe na kuwa ya mfano kwa kuwekewa mikakati mbalimbali ili iweze
kuwa na tija kwa mfugaji na taifa kwa ujumla pamoja na kuwataka wawekezaji
kuendeleza vitalu vyao kwa kuweka miundombinu imara bila kuwa na hofu ya uwepo
wa mkataba wa muda mfupi wa mwaka mmoja.
Nao baadhi ya wawekezaji katika Ranchi ya Kikukula
wameiomba serikali kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo
ya ufinyu wa maeneo ya mifugo yao huku wakiipongeza kwa namna inavyoboresha
sekta ya mifugo nchini.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya
Ranchi ya Taifa (NARCO) Prof. Phillemon Wambura akijibu hoja hizo amewataka
wawekezaji kuhakikisha wanapata vitalu kwa misingi ya kisheria.
Awali Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah
Ulega mara baada ya kuwasili mjini Bukoba alipata nafasi ya kukutana na mkuu wa
mkoa huo brigedia jenerali Marco Gaguti ambapo ameiomba Wizara ya Mifugo na
Uvuvi kufanya utafiti namna wafanyabiashara wanavyoweza kunufaika na mabaki ya
samaki yakiwemo mabondo.
Naibu Waziri Ulega yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya
kikazi ya siku tatu ambapo katika siku ya kwanza ametembelea ranchi za Kikulula
na Mabale pamoja na kuzungumza na wawekezaji katika ranchi hizo na kufanya
mkutano wa hadhara katika kijiji cha Katanda kilichopo Kata ya Kihanga,
Wilayani Karagwe.
No comments:
Post a Comment