Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. George Simbachawene
ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Pwagu
wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma katika mkujtano wa hadhara ulioambatana na
maombi maalumu alipofanya ziara ya kikazi.
..................................
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira), Mhe. George Simbachawene ameagiza taasisi ziwe
zinaandaa utaratibu wa upandaji miti wakati wa matukio au sherehe mbalimbali
hatua itakayohakikisha utunzaji wa mazingira unafanyika kwa ufanisi.
Pia amezitaka taasisi za umma, binafsi
na za dini kuhakikisha zinaandaa vitalu vya miche ya miti na kugawa kwa
wananchi waende kupanda akisema kuwa utaratibu huo utasaidia katika kuhakikisha
kunakuwa na ongezeko la miti nchini.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha
Pwaga wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Mpwapwa katika Jimbo la Kibakwe
Mkoani Dodoma, Mhe. Simbachawene alisema wastani wa ukataji miti kwa mwaka ni
496,000 ambao unatokana na shughuli za kibinadamu, hali inayochangia uharibifu
wa mazingira na kwa hali hiyo jukumu la kupanda miti ni la kila mtu.
“Nitafurahi kuona kiongozi yeyote
anapofanya ziara mahali popote anaandaliwa utaratibu wa kupanda miti halafu
ndio ahutubie mkutano na kwa kufanya hivyo tutaweza kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na kukosekana kwa miti na hapa Sheria ya
Mazingira ya Mwaka 2004 inasema kila mtu ni taasisi ya mazingira hivyo ni
lazima apande mti,” alisisitiza Waziri.
Kwa hali hiyo Mhe. Simbachawene ambaye
pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe alitahadharisha kuwa matumizi ya mkaa kwa
kiasi kikubwa yanachangia upotevu wa misitu yetu kwani unahusisha ukataji wa
miti ya asili ambayo huleta mvua na uaoto wa asili.
Aidha, katika ziara hiyo Kijijini hapo
pamoja na mambo mengine mara baada ya kuwasili Waziri huyo aliongoza zoezi la
upandaji miti kwenye eneo la Kituo kipya cha Afya cha Pwaga kwa pamoja na
viongozi mbalimbali Wilayani humo akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mpwapwa Paul Sweya.
Waziri huyo amebainisha kuwa shughuli
za kibinadamu ni nyingi na harakati za kutafuta maisha zinazosababisha akate
miti kwa wingi zimeongezeka na hivyo kumfanya aharibu mazingira kwa kukata miti
hivyo ni lazima sasa tulinde misitu yetu kwani ndio uhai wetu.
Kutokana na hilo aliwataka wananchi
kuacha mara moja kuvichezea vyanzo vya maji huku na kutaka uwekwe msukumo zaidi
kwa wananchi kuhusu suala zima la utunzaji mazingira na kuwa elimu itolewe
kuanza ngazi ya shule za msingi ili wanafunzi wapate uelewa.
“Miti ni muhimu sana kwani kusaidia
kupunguza mabadiliko ya tabianchi tena wataalamu wanasema ni vizuri kupanda
miti ya asili kwani ina uwezo mkubwa wa kunyonya hewa ya kaboni ambayo
ikiungana inatengeneza gesi joto ambayo inasababisha tabaka la ozone
linalosababisha joto kubwa duniani,” aliasa Mhe.Waziri.
No comments:
Post a Comment